19 July 2012
Tanzania kunufaika na utaalamu kilimo cha kisasa kutoka China
Na Imma Mbuguni, Changchun, CHINA
RAIS wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Jilin, Profesa Qin Guixin, kilichopo katika mji wa Changchun, nchini China, amesema chuo hicho kitaendelea kuzisaidia nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kwa kusambaza utaalamu wa kilimo cha kisasa.
Alisema lengo la chuo hicho ni kuhakikisha progamu ya mpango wa kuendeleza uhusiano kati ya nchi za Afrika na China inatekelezwa kwa vitendo ili kuchochea maendeleo zaidi.
Akizungumza mjini hapa juzi na mwandishi wa gazeti hili, Prof. Guixin, alisema nchi za Afrika zina uwezo mkubwa wa kupunguza majanga ya njaa kutokana na ongezeko kubwa la watu kama nchi hiyo ilivyoweza kufanikiwa.
“Miaka michache iliyopita, wataalamu wa kilimo kutoka Afrika walitembelea chuo chetu hapa Jilin, walishangazwa kuona jinsi Wachina tulivyoweza kuongeza uzalishaji wa chakula katika eneo dogo tu la ardhi,” alisema Prof. Guixin.
Alisema kutokana na mafanikio hayo, wataalamu hao walitoa mwaliko kwa wataalamu wa chuo hicho kuja Tanzania ili kufanya utafiti jinsi Afrika inavyoweza kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuiga teknolojia inayotumika nchini hapo.
Aliongeza kuwa, mahusiano ya chuo hicho na Afrika, yamechangia kufunguliwa Kituo cha Utafiti na Teknolojia nchini Zambia mwaka 2007 ambapo miaka mitano baadae, nchi hiyo itakuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo.
Prof. Guixin alisema mkakati wa chuo hicho kwa miaka mitatu ijayo ni kufanya utafiti, maonesho, kukuza teknolojia na kuendeleza mazao ya mahindi, maharage ya soya, uyoga na mbogamboga.
Akijibu swali la mwandishi wetu aliyetaka kufahamu ni jinsi gani Tanzania inaweza kutatua tatizo la njaa kwa kuiga teknolojia na kuongeza uzalishaji wa chakula, Prof. Guixin alisema chuo hicho kitaendelea kuzisaidia nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kwa kuwafundisha wataalamu wake kutumia teknolojia hiyo.
Chuo kikuu hicho chenye ukubwa wa ardhi hekta 1,500, kimeajiri wafanyakazi zaidi ya 1,800, ambapo walimu wa kudumu 1,051, kati yao,.walimu 499 ni Maprofesa
Pia chuo hicho kina wanafunzi 18,000, kati ya hao 15,875 wanasomea Shahada ya Kwanza ua Uzamili na 1,268 wanasomea Shahada ya Uzamili ambapo 126 PHD.
Mwandishi wetu pia alijionea kituo kikubwa kuliko vyote nchini humo ambacho kipo chini ya Wizara ya Elimu ambacho kinafanya tafiti mbalimbali.
China imeandaa ziara maalumu ambayo imeshirikisha baadhi ya waandishi kutoka Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa mkutano wa kuimarisha mahusiano kati ya China na nchi za Afrika.
Mkutano huo utafanyika leo na utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa bara la Afrika akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki-Moon, ambao utafanyika jijini Beijin.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment