09 July 2012

Saintfiet atambia mazoezi kutwaa Kagame



Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Tom Saintfiet amesema 'dozi' ya mazoezi aliyoanza kuitoa kwa wachezaji wake na nyingine itakayokuja ndio silaha pekee itakayosaidia timu hiyo kutetea ubingwa wa kombe hilo.

Kocha huyo ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo hivi karibuni, kibarua chake cha kwanza ni kuhakikisha anatetea ubingwa wa Kombe la Kagame.

Akizungumza wakati wa mazoezi ya timu hiyo juzi jioni kwenye Uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam, Saintfeit alisema mazoezi anayotoa ni ya kawaida ila ni magumu kwakuwa ni makocha wachache wanayotoa mazoezi ya aina hiyo.

"Nimefurahi kuona machezaji wanafanya kila ninachokitoa na hii inanipa hamasa kwamba tunaweza kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Kagame," alisema Saintefit na kuongeza;

"Na ndio maana ukiangalia mazoezi tunafanya kutwa mara tatu ili kuwaweka vizuri wachezaji wangu wawe na uwezo wa kucheza muda mwingi na baada ya kuona wapo vizuri nitarudisha katika programu ya kawaida."

Alisema muda uliobaki kwa ajili ya mashindano hayo ni mdogo na ndio maana ameamua kutumia muda mwingi kufanya mazoezi ya uwanjani na darasani ili aweze kwenda na muda.

Akizungumzia mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT Ruvu ambao utachezwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, alisema :"Nilisikia kutakuwa na mechi lakini sijui na timu ipi ila kama itakuwepo ni vizuri zaidi kwani itakuwa ni nafasi nzuri ya kuwaona wachezaji wangu."

No comments:

Post a Comment