18 July 2012

Madiwani Mbeya wakunjua makucha kwa watendaji


Na Esther Macha, Mbeya

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, limewafukuza kazi watendaji sita, wakiwemo watumishi watatu wa Idara ya Uhasibu kwa tuhuma za kujipatia fedha isivyo halali zaidi ya sh. milioni 35.3.

Akitoa tamko la kuwafukuza kazi mjini hapa jana kwenye kikao chao, Meya wa jiji hilo, Bw. Athanasi Kapunga, alisema baada ya madiwani kukaa kama kamati ili kuwajadili watumishi hao, walitoa pendekezo la watumishi hao kufukuzwa kazi.


Aliwataja watumishi hao kuwa ni Bi. Sarah Kibona (Mhasibu Mwandamizi), Bw. Tito Mwakisole (Mhasibu Daraja la Kwanza) na Bw. Petro Yohana, ambaye ni mlinzi.

Alisema Bi. Kibona na Bw. Mwakisole wanakabiliwa na shtaka linalohusu (kanuni 42), kujipatia fedha isivyo halali (wizi) zaidi ya sh. milioni 35.3 ambapo shtaka la pili linahusu (kanuni ya 42) kushindwa kutimiza wajibu hivyo kusababisha hasara.

“Watuhumiwa wote wanadaiwa kutumia vyeo vyao kwa kushirikiana na mtumishi wa Benki ya NMB, kuiba fedha za mishahara ya watumishi wasiostahili kulipwa kwa kuingiza mishahara hiyo katika akaunti zao na watu wengine.

“Kuhusu Bw. Bw. Yohana ambaye ni mlinzi, akaunti yake inadaiwa kutumiwa na watuhumiwa kwa kuingiziwa fedha zaidi ya sh. milioni 3.8 ambazo ni mali ya mwajiri.

Hata hivyo, Bw. Yohana anakabiliwa na shtaka la pili la kushindwa
kutimiza wajibu akiwa kama mlinzi wa Halmashauri ya Jiji hilo kwa kutotoa taarifa ya kuingizwa fedha hizo isivyo halali katika akaunti yake ili ziweze kurejeshwe serikalini.

Aliongeza kuwa, pia baraza hilo limependekeza Mthamini Ardhi Daraja la Pili Bw. Joseph Ndaki, afukuzwe kazi kwa tuhuma za kughushi taarifa za uthamini wa ardhi ili kuidanganya Serikali.

Alisema lengo la Bw. Ndaki ni kujipatia manufaa binafsi kutokana na fedha ambazo ingelipwa kama fidia ya eneo la Ikuti na Inyala kwa ardhi na mali ambazo hazipo.

Bw. Kapunga alisema Bw. Ndaki anadaiwa kushindwa kutimiza wajibu akiwa mtumishi, kuharibu taswira ya utumishi wa umma mbele ya jamii na kufanya vitendo vinavyodhalilisha akishirikiana na wananchi wasio waadilifu kughushi taarifa na kuidhalilisha Halmashauri ya Jiji hilo.

“Bw. Ndaki alikuza eneo la uthamini bila uhalali, hekta 72 ndizo alipaswa kuzifanyia kazi lakini yeye aliingiza hekta 190 kwa masilahi yake hivyo baraza limependekeza afukuzwe,” alisema.

No comments:

Post a Comment