09 July 2012

Polisi Dar kuunda timu ya Polisi Jamii



Na Heri Shaabaan

JESHI la Polisi linatarajia kuunda timu ya Mkoa wa Dar es Salaam katika mashindano ya Polisi Jamii ili iweze kutekeleza dhana ya polisi shirikishi karibu na wananchi.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mkuu wa Huduma za Polisi Jamii, Basilio Matei wakati wa kufunga mashindano ya polisi jamii ngazi ya kipolisi wilaya Kariakoo.

Matei alisema wanalipongeza Jeshi la Polisi Msimbazi kwa kuwa wa kwanza kubuni mbinu hiyo kuwashirikisha wananchi kushiriki mashindano hayo ambayo yalikuwa yakienda sambamba na kuwafundisha mbinu za Ulinzi Shirikishi.

"Washindi watakaopatikana katika mashindano haya watashiriki ngazi ya wilaya kipolisi Ilala hadi mkoa pia wakati huohuo tutakuwa tumefanikiwa kuwapa mbinu mbalimbali za ulinzi"alisema Matei.

Kwa upande wake Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Wilaya ya Kariakoo, Renatha Mzinga alisema mashindano hayo yalishirikisha timu sita za kata hiyo na lengo ni kuwapa elimu ya ulinzi,ajira kupitia sekta ya michezo na kujenga udugu.

Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza, Young Star alijinyakulia kombe na seti ya jezi,sh. 200,000 na mshindi wa pili, Kakayose alipata jezi seti moja mpira mmoja na sh. 15,0000 na mshindi wa tatu sh. 100,000.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime alisema amefurahishwa na wananchi kuitikia wito kushiriki mashindano ambayo baadae yataweza kuwaweka katika nafasi nzuri ambapo wakiendelea kushirikiana itakuwa njia yao ya kupata ajira na kujilinda wenyewe.

Aliwataka wasibweteke na kukaa vijiweni badala yake washiriki katika kazi mbalimbali zitakazoweza kuwaingizia kipato aidha hata kwa kubuni mradi.

No comments:

Post a Comment