09 July 2012

Kino, Dodoma zatinga robo Copa Coca-Cola



Na Janath Abdulrahim

TIMU za Kinondoni na Dodoma zimeingia robo fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012, baada ya kushinda mechi zao za 16 bora zilizochezwa jana jijini, Dar es Salaam.

Kinondoni imeitoa Rukwa baada ya kuichapa mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Karume ambapo mabao ya washindi yalifungwa na Yahya Mohamed dakika ya 13, Issa Ally dakika ya 44 na Mabrouk Liyayala dakika ya 80 na Ladislaus Fwamba aliifungia Rukwa dakika ya 46.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kwa ushindi huo, Kinondoni itacheza robo fainali ya tatu kesho Uwanja wa Karume dhidi ya mshindi wa mechi ya 16 bora kati ya Kilimanjaro na Mwanza iliyochezwa jana jioni.

Alisema Dodoma imenyakua tiketi ya kucheza robo fainali baada ya kuifunga Arusha bao 1-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers.

Alisema bao la washindi lilifungwa dakika ya tano kabla ya filimbi ya mwisho na Ayoub Khalfan.

Katika robo fainali, Dodoma itacheza na mshindi wa mechi ya 16 bora kati ya Tabora na Tanga italiyochezwa jana jioni Uwanja wa Tanganyika Packers.

Robo fainali zote zitachezwa Uwanja wa Karume ambapo ya kwanza itafanyika kesho asubuhi kati ya Temeke na Mjini Magharibi wakati jioni itakuwa Mara na Morogoro.

No comments:

Post a Comment