17 July 2012
Ni Morogoro Copa Coca-Cola
Na Janath Abdulrahimu
TIMU ya Morogoro imeibuka bingwa wa michuano ya Copa Coca-cola baada ya kuichaliza Mwanza bao 1-0 katika mechi iliyochezwa jana jioni kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Bao lililoipa ubingwa Morogoro, lilifungwa na Salum Ramadhani dakika ya 35 na kuifanya timu hiyo kutawazwa mabingwa wapya wa michuano hiyo ambapo walipata zawadi ya sh. milioni 8 na medali ya dhahabu.
Katika mechi ya mshindi wa tatu iliyochezwa saa tano asubuhi kwenye uwanja huo huo, Temeke aliichapa Tanga kwa mabao 2-0, hivyo kushika nafasi ya tatu.
Mabao ya Temeke yalifungwa na Rehani Kibingu dakika ya 48 na 82 ambapo walizawadiwa sh. milioni 3 na medali na Mwanza ambayo imeshika nafasi ya pili ilipata sh. 4,800,000 na medali.
Katika mechi hiyo ya fainali, timu zote zilionesha kandanda safi kwa kushambuliana kwa zamu kila kipindi lakini mpaka dakika 90 zikimalizika Morogoro iliibuka bingwa wa michuano hiyo.
Akizungumzia matokeo hayo, Kocha wa Morogoro, Mecky Mexime alisema timu yake imecheza vizuri japo ilionesha udhaifu kipindi cha kwanza na kwamba ameyapokea vizuri matokeo hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment