23 July 2012

Ni kazi ngumu timu zetu kutwaa Kombe la Kagame mwaka huu


Na Nyakasagani Masenza

TIMU za Tanzania zinazoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati 'Kagame Cup', zinakabiliwa na mtihani mgumu wa kutwaa tena kombe hilo mwaka huu kutokana na ushindani mkali unaooneshwa na timu zinazoshiriki.


Michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na kati (CECAFA), inafanyika kwa mara nyingine nchini Tanzania kwa udhamini wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Yanga na Simba zilizokuwa na matumaini makubwa, zilianza michuano hiyo kwa kufungwa idadi sawa ya mabao na wapinzani wao, katika michezo wa awali na kuonesha kiwango cha chini kwenye michuano hiyo, inayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pamoja na ushindi wa mabao 7-1, waliopata Mabingwa watetezi wa Kombe hilo, Yanga ya Tanzania Bara, dhidi ya Wau Salamu ya Sudan Kusini na 3-0, walizopata Simba kwa Ports FC ya Djibout, ushindi huo siyo kigezo kwa timu hizo kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Iwapo wachezaji wa timu hizo wataendelea kucheza soka la upande mmoja kama walivyocheza katika michezo iliyopita, itakuwa vigumu kupata ushindi.

Wau Salamu na Ports ni timu dhaifu katika michuano hiyo, hivyo Yanga kuishinda timu hiyo kwa mabao 7-1 na Simba kupata mabao 3-0 si kiwango cha kuridhisha kwa timu hizo kufanya vizuri mwaka huu.

Katika michezo yao ya awali, Yanga walichapwa mabao 2-0 na Atletico ya Burundi, katika mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo nao Simba wakiambulia kipigo kama hicho kutoka kwa wakusanya mapato URA ya Uganda.

Wakati vigogo wa soka la Tanzania, wakipata kipigo katika michezo yao ya awali, Azam na Mafunzo kutoka Zanzibar zilishindwa kutambiana, zilipocheza kwenye uwanja wa Chamazi na kufungana 1-1.

Wau Salamu ya Sudan Kusini, ambayo ni timu ngeni katika mashindano hayo na Ports ya Djibout iliyoshiriki mara kadhaa, hazina viwango vizuri vya kuonesha matumaini kwa timu zinazotegemewa na watanzania kama Yanga na Simba.

Viwango vya juu vilivyooneshwa na wachezaji wa timu za URA, Atletico, Vita ya Congo na APR ya Rwanda, inaweza kuwa kikwazo kwa timu za Tanzania, kutwaa kombe hilo.

Tanzania Bara inawakilishwa na timu tatu, ambazo ni mabingwa watetezi Yanga, mabingwa wa Tanzania Bara Simba na Azam, huku timu pekee kutoka Visiwani Zanzibar ni Mafunzo.

Inawezekana timu za Tanzania zikafuzu kuingia hatua ya robo fainali kwa kubahatisha, kutokana na ushindani ulivyo katika makundi, lakini kama hazikujipanga vizuri, zinaweza kuondolewa mapema katika hatua inayofuata.

Ili timu zetu ziepuke kuwa wasindikizaji katika michuano hiyo, zinapaswa kujipanga kikamilifu kwa kubaini udhaifu uliopo, kwani zote zinafundishwa na makocha wenye sifa, ambao ni Tom Saintfiet wa Yanga, Milovan cirkovic wa Simba na Stewart Hall wa Azam.

Wakati Yanga, Simba, Azam na Mafunzo zinakabiliwa na mtihani mkali wa kutwa kombe hilo, Simba wamepata pigo baada ya beki wake wa kushoto, Amir Maftah kuumia na kutakiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili.

Timu zinazoshiriki michuano hiyo mwaka huu ni mabingwa watetezi Yanga, Simba na Azam za Tanzania Bara, APR ya Rwanda, Tusker Kenya, Mafunzo Zanzibar, URA Uganda, Atletico Burundi, Vita Congo, Ports Djibout na Wau Salamu Sudan.

No comments:

Post a Comment