30 July 2012
Mnyika: Nipo tayari kutoa ushahidi wa Nchimba
Na Stella Aron
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo Bw. John Mnyika, amesema yupo tayari kutoa ushahidi wa tuhuma alizotoa dhidi ya Mbunge wa Iramba Magharibi, Bw. Mwigulu Nchimba (CCM).
Alisema anachosubilia kwa sasa ni kuitishwa kikao cha Kamati ya Kanuni ya Bunge ili aweze kuwasilisha ushahidi unaomuhusu Bw. Nchemba, kuhusika na ufisadi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Taarifa aliyotolewa na Bw. Mnyika kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema hatua hiyo imelenga kudumisha ukweli na kuhakikisha Bunge linaendeshwa kwa kanuni bila upendeleo ili kutimiza wajibu wa kikatiba na kuisimamia Serikali kwa ufanisi.
Alisema Mwenyekiti wa Bunge, Bi. Jenister Mhagama, alimtaka kuwasilisha ushahidi wa tuhuma alizotoa kwa Bw. Nchemba ambapo pamoja na kuomba muda ili aweze kuzitaja tuhuma hizo, hakupewa fursa hiyo.
“Badala yake Bi. Mhagama ambaye alikuwa anaendesha shughuli za Bunge siku hiyo, alinipa siku saba za kutoa ushahidi bungeni na tayari nimewasilisha kwa Spika Bi. Anne Makinda ushahidi wa awali kuhusu tuhuma ambazo nilizitoa,” alisema.
Bw. Mnyika alidai kushangazwa na miongozo mbalimbali ambayo imetolewa siku za nyuma lakini haipatiwi majibu hadi sasa.
“Nimeshawasilisha barua yangu kwa mujibu wa Kanuni ya 5 (4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge tangu Julai 12 mwaka huu, dhidi ya uamuzi wa Mwenyekiti wa Bunge Bi. Mhagama ambao kimsingi haukuzingatia matakwa ya kanuni za kudumu na uendeshaji bora wa Bunge.
“Ninachosubiri sasa ni Spika kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kulijulisha Bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa,” alisema.
Alisema ameamua kukata rufaa kwa sababu tatu, moja ni Mwenyekiti kumtaka kuwasilisha ushahidi wa suala ambalo hakulisema yeye bali amelisema yeye.
Sababu ya pili ni kutopewa nafasi ya kueleza tuhuma alizotaka kueleza dhidi ya Bw. Nchemba badala yake Mwenyekiti aliendelea kumtaka azungumzie tuhuma alizozieleza yeye.
Tatu Mwenyekiti hakufanya uamuzi kuhusu suala ambalo yeye aliliombea kuhusu utaratibu kwa mujibu wa kanuni ya 64 (1) (a) kuhusu madai ya Bw. Nchemba juu ya hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Ofisi ya Rais.
Alisema katika barua yake kwa Katibu wa Bunge, ameeleza ni muhimu Kamati ya Kanuni ikakutana kabla Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kushughulikia uamuzi uliofanywa na Naibu Spika Bw. Job Ndugai, Julai 12 mwaka huu, kwenye kikao cha 22 cha Mkutano wa nane.
“Kamati ya Kanuni ndiyo itashughulikia ushahidi huu na kuthibitisha kama Bw. Nchemba alihusika na wizi wa fedha za EPA, ili kamati isifanye uamuzi kwa kurejea mwongozo usiokuwa sahihi.
Bw. Mnyika alisema pamoja na kuwawakilisha wananchi katika masuala mengine ya maendeleo bungeni, hatua ya kukata rufaa imelenga kudumisha ukweli na kuhakikisha Bunge linaendeshwa kwa kuzingatia kanuni bila upendeleo ili kutimiza wajibu wa kikatiba wa kuisimamia Serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment