17 July 2012
Milovan kukifumua kikosi Simba
Na Zahoro Mlanzi
BAADA ya kuchapwa mabao 2-0 na timu ya Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) katika michuano ya Kombe la Kagame, Kocha Mkuu wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara Simba, Milovan Cirkovic amesema atakipangua kikosi kilichoanza katika mechi hiyo.
Timu hizo zilikutana juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa mechi za kwanza za michuano hiyo, ambapo mabao ya URA yalifungwa na Feni Ali katika kila kipindi.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Milovan alisema lazima akifanyie mabadiliko kikosi hicho kwani kimeonekana kina upungufu mkubwa na ndiyo maana wamepoteza mchezo huo.
"Nitafanya mabadiliko kwa baadhi ya maeneo, ila nimeshagundua makosa tuliyofanya hivyo mabadiliko hayo yatakwenda sambamba na kubadili kikosi changu kiwe na ushindani zaidi," alisema Milovan.
Akijibu swali kuhusu kiwango kikubwa kilichooneshwa na beki wake wa zamani, Derick Walulya katika mechi hiyo, Milovan alisema: "Sijutii kumuacha Walulya ila ni mchezaji mzuri na ameonesha kiwango kizuri katika mechi ile."
Alisema ni mchezaji mzuri lakini kwa wakati ule hakuwa katika kiwango kizuri na inawezekana amecheza kwa bidii kwa kutaka kuionesha timu yake ya zamani jinsi alivyo vizuri.
Mabingwa hao wa Bara watashuka tena uwanjani kesho kuumana na Ports ya Djiobuti katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ports katika mechi ya kwanza ilichapwa mabao 7-0 na Vita Club ya Jamhuri ya Kidekrasi ya Congo (DRC).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment