Na Grace Ndossa
MIGOGORO ya ardhi ambayo inaibuka mara kwa mara inachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya sekta ya kilimo na kuendelea kuangamiza zaidi ya asilimia 70 ya watanzania ambao huishi kwa kutegemea kilimo.
Hali hii inatokana na ukweli kuwa zaidi ya watanzania wanategemea kukuza uchumi wao kupitia kilimo ambacho hutegemea ardhi.
Sambamba na kilimo pia jamii kubwa ya wananachi hutegemea ardhi kwa ajili ya kufuga mifugo yao na kujipatia mahitaji yao ya kila siku.
Hali ya kuwepo kwa migogoro ya ardhi ya mara kwa mara katika sehemu mbali mbali za Tanzania inachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma ufanisi katika sekta za kilimo na mifugo na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti ya kutetea Haki za Ardhi Bw. Yefred Miyenzi anasema kuwa kutokana na utafiti waliofanya mji wa kigamboni tangu serikali ilipobuni mradi wa kuanzisha mji mpya mwaka2008 wamebaini athari mbali mbali zilizotokea tangu kusitishwa kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Anasema kuwa kutokana na hali hiyo waliamua kufanya utafiti maalum juu ya athari , kijamii na kimazingira zilizotokana na kuanzishwa kwa mradi huo tangu 2008 hadi sasa na athari za kimazingira endapo hali hiyo haitarekebishwa kutokana na matokeo ya utafiti huo.
Anaelezea kuwa utafiti huo uliongozwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Kampasi ya Dar es salaam Profesa Sist Joseph akishirikiana na Bi Rosemary Mramba kutoka Taasisi ya ushauri wa masuala ya maendeleo na jamii (FOSSTAN).
Bw. Miyenzi anasema kuwa utafiti huo ulianza Disemba mwaka jana hadi Machi 2012 ulioshirikisha watu mbali mbali wakiwemo ngazi za serikali za mitaa kata na halmashauri husika wananchi wa kigamboni Ofisi iliyoratibu mradi huo katika Wizara ya Ardhi.
Anasema kuwa utafiti huo ulibaini kuwa shughuli za uchumi zimesimama kwa muda mrefu na kusababisha wananchi wanaotegemea kilimo upandaji wa mihogo mbogamboga kudorora na nyingine kufa kabisa na hivyo kuathiri kipato kwa kaya zilizokuwa zikijikimu kutokana na shughuli hizo.
Pia anasema kuwa kukosekana kwa mikopo kutoka taasisi za kifedha kwa dhamana ya mali kwani wananchi walio wengi walikuwa wanatumia ardhi yao kuweka rehani ili waweze kupata mikopo na kuendeleza shughuli za kiuchumi pamoja na kusomesha watoto lakini tangu kusitishwa kwa shughuli hicho maisha yao yameyumba kiuchumi.
Hata hivyo anasema kuwa tangu kutolewa kwa tamko hilo kasi ya wapangaji wa makazi imekuwa ikipungua wakiwa na imani kuwa mradi unaweza kuanza muda wowote na wapangaji wanapopatikana hawakubali mikataba ya muda mrefu na badala yake hulipa kodi ya pango ya mwezi mmoja
Bw. Miyenzi anasema kuwa tangu tamko hilo litolewe la kusitisha maendeleo katika eneo la mradi kigamboni ilikuwa inakua kwa kasi kutokana na ujenzi wa majengo mapya hasa kwa ajili ya makazi
Pia utafiti huo ulibaini kuwa baadhi ya majengo ambayo watu walikuwa wakijenga kabla ya kutolewa kwa amri ya zuio yamebaki bila ya kuyaendelezwa, hii imeathiri kwa kiasi kikubwa mategemeo ya wananchi ya kujipatia kipato endapo wangeweza kumaliza majengo yao.
Hata hivyo vijana wengi wamekosa fursa za ajira bila ya kuwa na njia mbadala ya kupata kipato kwani hii inachangi idadi kubwa ya vijana kujiingiza katika matukio na matendo ya uvunjaji wa sheria kama vile uporaji , ukabaji na matumizi ya madawa ya kulevya.
Anasema kuwa mzunguko wa kifedha umepungua kutokana kupungua kwa shughuli za uzalishaji pamoja na wategemezi wa shughuli za msingi za kiuchumi pamoja na wauzaji wa vyakula kwa wafanyakazi .
Bw. Miyenzi anasema kuwa kumekuwapo na athari za kisaikolojia kwa baadhi ya wakazi wa Kigamboni kwani jamii imeshindwa kutabiri nini hatima yao majengo ambayo hayajakamilika watu hawana vipato vya kujikimu hawajui fidia itatoka lini, kutokana na mfumo wa uthamini hauko wazi na taarifa haziwafikii kwa wakati.
Katika utafiti huo wakazi wa kigamboni walieleza kuwa serikali haijawa wazi na wananchi wa eneo hilo hawajui faida ya huo mradi kwao na bado wana hofu ya kuwa wageni katika ardhi yao na kutaka kujua nini wajibu wao na kwa muda gani wakae wakisubiri.
Wanaeleza kuwa baada ya amri ya zuio kuisha muda wake baada ya miaka miwili hakujawa na taarifa za wazi kuwaambia nini kinachoendelea licha ya kusikia tu mijadala bungeni na kwenye vyombo vya habari kwani kinachotakiwa ni uwazi katika kutekeleza mradi hatua kwa hatua badala ya kuwaacha wananchi wakipiga ramli kubashiri nini kitatokea.
Pia anasema kuwa wakazi wa kigamboni wanahitaji kushirikishwa kikamilifu kujadili na kutoa mawazo yao kwa njia ya vikao halali kama wamiliki wa ardhi sheria ya mipango miji inawatambua kama wadau muhimu na kama siyo serikali inayotaka kuwekeza kwanini wawekezaji wasingekwenda wao wenyewe moja kwa moja kujadili na wananchi.
Anasema kuwa malipo ya fidia kamili na ya haki kwa wakati anaeleza kuwa uzoefu unaonesha kuwa katika miradi mingine kuwekuwa na tatizo la ulipwaji fidia kwani wananchi wanataka kuona zoezi la uthaminishaji mali na rasilimali zao linakuwa na wazi na ushirikishwaji unatakiwa ili hatimaye fidia iweze kuwa ya haki kulingana na viwango vya soko.
Hata hivyo anasema kuwa kuna haja ya kuangalia fidia ilipwe kwa kuzingatia bei ya soko lililopo hivi sasa badala ya kufanya tathimini kwa kutumia bei ya zamani ambayo inaangali thamani ya wakati huo ya sarafu .
Bw.Miyenzi anasema kuwa kutokana na utafiti huo madai ya wananchi kutokana na matokeo ya utafiti huu yazingatiwe na kufanyiwa kazi ili haki itendeke na wananchi wasibaki kuwa wahanga wa maendeleo badala ya kunufaika nayo, Suala la ushirikishwaji wa wananchi katika kila hatua linapaswa kupewa kipaumbile kwani kukosekana kwake ndicho kiini cha migogoro mingi ya ardhi isiyokwisha mijini na vijijini.
Pia serikali inatakiwa kujenga utamaduni wa kuheshimu haki za wenyeji kwenye ardhi badala ya mara zote kuwachukulia kama watu wasio stahiki wakati wamewekeza nguvu kazi zao mali na rasilimali zao na fidia itazamwe upya badala ya kutolewa kwa mkupuo mara moja inaweza kutolewa kwa awamu na kushirikisha vitu visivyo pesa taslimu kama vile ubia katika miradi.
No comments:
Post a Comment