27 July 2012

Mgomo wa walimu sasa wanukia *Unaratibiwa na CWT, kura zaanza kupigwa


Na Reuben Kagaruki, Kagera

SERIKALI imeshindwa kufikia muafaka na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), juu ya madai yao kupitia Tume ya Usuluhishi ambapo hivi sasa wanachama wa chama hicho wameanza kupewa barua ili wajiandae kwa mgomo baada ya taratibu kukamilika.

Majira limeshuhudia barua zilizosambazwa mkoani Kagera ambazo zinazowaeleza walimu juu ya kukwama kwa mazungumzoa katia ya chama hicho na Serikali pamoja na kutoa mwongozo wa mambo yanayotakiwa kufanyika ili kufanikisha mgomo huo.

Kwa mujibu wa barua hiyo yenye namba CWT/004/MM/VOL.III/23 ambayo imetolewa Julai 20 mwaka huu, inawataka walimu kujiandaa kupiga kura za ndio au hapana ili kuridhia kufanyika au kutofanyika kwa mgomo huo.

Barua hiyo ambayo imesainiwa na Katibu Mkuu wa CWT, Bw. Ezekiah Oluoch, ilidai kilichokuwa kikisubiriwa kabla ya kupiga kura za kubariki mgomo ni cheti kutoka kwa Mwenyekiti ambaye ameteuliwa na Tume ya Usuluhishi, Bw. Msigwa ili kuonesha muafaka umeshindikana kati ya pande hizo.

“Mgogoro huu umeshindikana kutatuliwa hivyo pande mbili zinaposhindwa kuelewana kwenye mgogoro wa kimasilahi kwa mujibu wa kifungu cha 80 (1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, chama cha wafanyakazi kinatakiwa kupiga kura ili kuamua wagome au la,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo, barua hiyo ilisema kura haiwezi kupigwa hadi msuruhishi atoe cheti kinachoonesha pande mbili zimeshindwa kufikia muafaka ambapo CWT ikikipata, itatoa mwongozo kuhusu hatua za kupiga kura.

Nakala za barua hiyo zilikuwa zikisambazwa katika shule mbalimbali mkoani hapa na Matibu wa CWT Wilaya ambayo ilisisitiza kuwataka walimu kuzingatia mwongozo ambao utatolewa na chama hicho wakati wowote.

Barua hiyo iliagizwa kuhamasishwa walimu kupiga kura bila woga na kuepuka vitisho vya Serikali ambavyo vitafuata baada na kabla ya kupiga kura hizo.

Makatibu wa Wilaya walitakiwa kuandaa bahasha za kutunzia kura kwa kugonga muhuri wa Wilaya husika na idadi ya kura zilingane na idadi ya wanachama husika.

Hata hivyo, barua hiyo ilionya kuwa ni kinyume cha sheria kupiga kura kabla ya tarehe ambayo itatangazwa na Mwenyekiti wa CWT, Bw. Gratian Mukoba.

Hivi karibuni, CWT ilitangaza mgogoro na Serikali ambao ulisajiliwa kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Juni 8 mwaka huu na kupewa namba A/DSM/ILA/369/12.

Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka vyanzo vya kuaminika, zinasema Mwenyenyekiti wa Tume ya Usuluhishi alihitimisha majadiliano hayo kwa kueleza kuwa, msimamo wa pande mbili baina ya CWT na Serikali unaonesha kukwama kutatuliwa.

Wakati huo huo, Waandishi Mariam Mziwanda na Tumaini Maduhu, wanaripoti kuwa, CWT kimeanza mchakato wa upigaji kura kwa ajili ya kushinikiza mgomo huo kutokana na tume hiyo kuwapa cheti cha kushindwa kusuruhisha mgogoro huo.

Akizungumza na Majira, Bw. Mukoba alisema Julai 25 chama hicho na Serikali walifika kwa msuluhishi Bw. Cosmas Msigwa ambaye ameteuliwa na tume kutatua mgogoro huo ambao umeshindikana.

“Kazi ya kupiga kura imeanza toka jana na inaendelea hadi kesho saa tatu asubuhi, kura zitapigwa mchana na usiku ili kutoa maamuzi ya wanachama kama wanagoma au la,” alisema Bw. Mukoba.

Aliongeza kuwa, mgogoro huo unahusu masilahi ya walimu likiwemo ongezeko la kima cha chini cha mishahara lakini chama hicho kinashangazwa na tamko la Serikali kuitaka CWT kuwakilisha takwimu za walimu wanaopaswa kulipwa ili ifanye hesabu kwani hawajui walimu wangapi wanastahili kulipwa.

Bw.Mukoba alisema, hoja hiyo ni yakupotosha ukweli wa madai ya waalimu kwani Serikali ina takwimu za matumizi ya zaidi ya trilioni nne kwa ajili ya kulipa mishahara ya waalimu kwa viwango.

Kwa Upande wake, Bw. Oluoch alisema, baada ya kukamilika kwa kazi ya upigaji kura, Baraza la Taifa la CWT litakutana kwa dharura kutangaza aina ya mgomo, muda utakaotumika sambamba na kutoa notisi ya saa 48 kwa Katibu Mkuu Kiongozi alinde mali zake.

Aliwataka wanachama wa chama hicho kuunga mkono ongezeko la mishahara asilimia 100, posho yakufundishia walimu wa sayansi kwa asilimia 55, asilimia 50 kwa walimu wa sanaa na posho ya mazingira magumu asilimia 30.


1 comment:

  1. NI KWELI TUNA MATATIZO WAALIMU TUNA VYOMBO VINGI VINAVYOSHUGHULIKIA MASILAHI YA WAALIMU TSD ,TSC NA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU AU MKURUGENZI MKOA SASA TUNACHANGANYIKIWA KWANZA SOLIDARITY KATI YA WAALIMU WA MSINGI,SEKONDARI NA VYUO VYA UALIMU HAIPO TUNAOMBA ANAYETAKA UMAARUFU KISIASA AKOME KUTUTUMIA WAALIMU KAMA NGAZI KUPANDISHA MSHAHARA TU SI TIJA IWAPO KODI YA MAPATO AU VAT ITAKATWA KWENYE MISHAHARA HIYO

    ReplyDelete