23 July 2012

Mbunge ajisafisha tuhuma ya bilioni 2/-



Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalumu, Bi. Anna Abdallah (CCM), jana alitoa ufafanuzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za Bodi ya Korosho sh. bilioni 2 zinazodaiwa kutumiwa na wajumbe wa bodi hiyo kwa kulipana posho za vikao badala ya kuendesha sekta hiyo.


Bi. Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa bodi hiyo nchini, aliyasema hayo mjini Dodoma jana siku moja baada ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Bi. Rose Kamili, kumlipua ufisadi huo na kudai bodi hiyo inatumia fedha za wakulima wa zao hilo kulipana posho.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo, Bi. Abdallah alisema sh. bilioni 2, zinazodaiwa kutolewa ili kuendesha sekta hiyo si kweli bali zaidi ya sh. bilini 13, zilitolewa kuendesha zao hilo.

“Ukweli ni kwamba, sh. bilioni 2 ambazo zinadaiwa kufujwa, si za kuendeshea kilimo cha korosho isipokuwa kwa shughuli za bodi pamoja na vikao, watu waliochomoa fomu ya malipo na kumkabidhi Bi. Kamili wamefanya vitendo vibaya ndani ya Serikali kwa kuvujisha nyaraka,” alisema.

Akizungumzia mke wa mjumbe wa bodi hiyo, Bw. Mudhihir Mudhihir kulipwa posho wakati hakustahili Bi. Abdallah alitetea na kusema aliteuliwa na mjumbe huyo kuwa msaidizi wake hivyo alistahili kulipwa posho kwa kazi aliyofanya kutokana na matatizo ya mkono aliyonayo.

“Si kweli kwamba mke wa Bw. Mudhihir ni mjumbe wa bodi, yeye ndio msaidizi wake kama amelipwa sikatai lakini sio mjumbe ni msaidizi, mwenyewe amemchagua mkewe amsaidie sasa nongwa iko wapi,” alisema Bi. Abdallah.

Kuhusu Bw. Jerome Bwanausi kulipwa mara mbili Bi. Abdallah alisema alifanya kazi siku za nyuma bila kulipwa ambapo siku hiyo ya kikao alistahili kupewa malipo hayo.

Aliongeza kuwa, matatizo yaliyopo katika zao hilo hayasababishwi na bodi bali ubinafsishaji wa viwanda usiozingatia uendelezaji ambao umechangia kuua zao hilo.

Alisema viwanda vingi vya korosho havifanyi kazi ambapo zao hilo limekuwa likisafirishwa kwenda nchini India ambako shughuli zote hufanyika huko.

“Viwanda hivi virejeshwe tuweze kubangua korosho nchini kwetu ili kutoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi,” alisema Bi. Abdallah.

1 comment:

  1. mudhihir mgonjwa msaidizi wake analipwa na bodi kwa utaratibu upi? kama sio ufisadi. wapo wa tz ambao wanaweza kuwa wajumbe sio lazima awe mudhihir apumzike wengine wapate nafasi ya kuongoza.tubadilike jamani ili tupate maendeleo kwa haraka kuliko hii ya kupeana ulaji inatuludisha nyuma kimaendeleo.ILI TUENDELEE TUNAHITAJI VITU 4 WATU.ARDHI.SIASA SAFI.NA UONGOZI BORA!!!!!

    ReplyDelete