11 July 2012

Mbunge adai bil. 19/- haimalizi tatizo la maji


Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Mkinga, mkoani Tanga, Bw. Dunstan Kitandula (CCM), amesema kitendo cha Serikali kutenga sh. bilioni 19 kwa ajili ya maendeleo ya maji, haiwezi kumaliza tatizo linalowasumbua wananchi wa jimbo hilo kwa miaka mingi sasa.


Alisema wananchi wa jimbo hilo wamechoshwa na mipango ya Serikali wakati shida ya maji ikiendelea kuwaumiza hivyo ameitaka isiridhike na Mafanikio ya Malengo ya Milenia, kwenye sekta ya maji kwani hali za wananchi vijijini ni mbaya.

Bw. Kitandula aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akichangia Bajeti ya Wizara hiyo na kusisitiza kuwa, Machi mwaka huu, Dunia ilisherehekea kufikia Malengo ya Milenia katika sekta ya maji.

Alisema kwa mujibu wa Taarifa za Mashirika ya Kimataifa WHO na UNICEF, yalionesha asilimia 89 ya wananchi ulimwenguni kote wanapata maji safi na salama.

Aliongeza kuwa, Tanzania iko nyuma kwa upatikanaji wa maji ambapo takwimu zinaonesha kuwa, Tanzania ni nchi ya 168 kati ya 179 kwa upatikanaji wa maji.

Alisema upatikanaji wa maji nchini ni asilimia 53, kiwango ambacho hakiendani na mahitaji ya wananchi hasa vijijini.

“Wananchi wa Mkinga kwa miaka 50 sasa, wanasubiri huduma ya maji kupitia mradi wa vijiji 10 lakini licha ya Wilaya hii kuwa miongoni mwa halmashauri zilizokidhi vigezo vya kuchimbiwa visima, hadi sasa imekuwa kitendawili.

“Kijiji kimoja tu cha Daluni ndicho mradi wa maji umeanza kutekelezwa, Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga yanashindwa kuendelezwa shughuli za ujenzi kutokana na ukosefu wa maji tangu ianzishwe mwaka 2006,” alisema.



No comments:

Post a Comment