17 July 2012
Mashabiki Yanga roho kwatu *Ni baada ya Simba kufungwa 2-0 *Azam, Mafunzo zakabana, Vita yaua
Na Zahoro Mlanzi
BORA matokeo haya, jiji sasa litatulia!ndivyo walivyosikika mashabiki wa timu Yanga baada ya mshambuliaji wa Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA), Feni Ali kufunga bao la pili dakika ya 90 na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa wa Bara, Simba.
Mechi hiyo ilipigwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maelfu ya mashabiki wa Simba ambao waliupamba uwanja huo kwa nguo zao nyekundu walizovaa.
Katika mechi hiyo ambayo ililazimika kuongezwa kwa dakika nne za ziada kutokana na muda mwingi kupotea kwa wachezaji wa timu hizo kuumia, ndizo zilizoifanya URA kuibuka na ushindi huo ambao unaonekana kupokelewa vizuri na mashabiki wa Yanga waliokuwepo uwanjani hapo kuishangilia.
Kwa matokeo hayo, inazifanya timu wenyeji Simba na Yanga kuanza vibaya Kombe la Kagame ambapo Yanga nayo ilifungwa kwa idadi kama hiyo na Atletico ya Burundi huku mwenyeji mwingine, Azam ikitoa sare na Mafunzo ya Zanzibar ya bao 1-1.
Mabao ya URA yalifungwa na Ali katika kila kipindi ambapo la kwanza alifunga dakika ya 11 kwa kichwa akiunganisha krosi safi ya Owen Kasule na la pili dakika ya 90 pia kwa kichwa akimalizia mpira uliopigwa na nahodha, Massa Simeon.
Mechi hiyo ilikuwa na ushindani wa aina yake ambapo timu zote zilicheza soka la aina moja la kupiga pasi nyingi eneo la katikati, Simba mara nyingi ilikuwa ikipenyeza mipira yake katikati lakini ilikwama kutokana na kizingiti cha Derick Walulya, mchezaji waliyemuacha msimu uliopita.
Walulya alionekana kumdhibiti vizuri Felix Sunzu na Danny Mrwanda kwani kila mipira iliyokuwa ikipigwa kwake aliiokoa na wakati mwingine alipanda mbele kuongeza mashambulizi.
Katika mechi hiyo, Simba itajutia nafasi ilizopata dakika za 5, 11 na 38 kupitia kwa Sunzu na Mwinyi Kazimoto ambapo mashuti waliyopiga yaliokolewa na kipa, Mugabi Yasin huku Robert Ssentongo wa URA naye alimpa wakati mgumu Juma Nyosso kwa jinsi alivyokuwa akimsumbua.
Katika mechi zingine zilizopigwa jana kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliibugiza Ports ya Djibout mabao 7-0.
Mabao ya Vita yalifungwa na Etekiana Taddy dakika za 14, 30, 74 na 84, Ngudikana Emmanuel alifunga dakika za 21 na 34 na Basilisa Makola alifunga dakika ya 13.
Mechi iliyofuata ilikuwa kati ya Azam FC dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 ambapo bao la Azam lilifungwa na John Bocco dakika ya 27 na dakika ya 47, Ally Hassan aliisawazishia Mafunzo.
Simba:Juma Kaseja, Haruna Shamte, Amir Maftah, Obadia Mungusa, Nyosso, Musa Mudde, Sunzu, Amri Kiemba/Uhuru Seleman, Kazimoto, Mrwanda/Abdallah Juma na Kanu Mbiyavanga/ Haruna Moshi 'Boban.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment