19 July 2012
'Malaria inaongoza kwa kuua Afrika'
Na Goodluck Hongo
BARA la Afrika linaongoza kwa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria kwa asilimia 89 na asilimia 83, wanaugua ugonjwa huo ambapo jitihada za kupunguza vifo hivyo, zimefanikiwa kwa asilimia 33.
Mwenyekiti wa kwanza wa Taasisi ya African Leaders Malaria Alliance-ALMA, ambaye alimaliza muda wake, Rais Jakaya Kikwete, aliyasema hayo Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa, Bara la Afrika linaloongoza kwa vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa huo.
“Baada ya kubaini ugonjwa huu ni hatari, nilitoa wazo kwa viongozi wenzangu wa Afrika kuungana ili kutokomeza ugonjwa huo, lengo la kuanzishwa ALMA ni kuwataka viongozi husika kushirikiana ili kupambana na malaria,” alisema.
Alisema Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya wanawake na watoto walio chini ya miaka mitano kwa silimia 50 ambapo Zanzibar imefanikiwa zaidi kutokomeza ugonjwa huo.
“Hivi sasa Serikali ina mpango wa kupiga dawa kila nyumba ili kutokomeza ugonjwa huo, hadi sasa vyandarua milioni 400 tayari vimetolewa baada ya Tanzania kupata vyandarua milioni 17.
“Kati ya hivi, milioni tisa vilitolewa kwa watoto ambapo ALMA itawezesha kupatikana dawa za kutibu ugonjwa huu kwa bei nafuu,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake, Rais wa Liberia ambaye ndiye Mwenyekiti wa ALMA, Bi. Ellen Johnson Sirleaf, alisema malengo ya ALMA yalikuwa hadi kufikia 2015, wagonjwa na vifo vya malaria vifikie asilimia 0.5 lakini kutokana changamoto ambazo zimejitokeza, wataongeza miaka mitano hadi 2020 kufikia lengo hilo.
Alisema nchi nyingi za Afrika zimeathirika kutokana na ugonjwa huo hivyo kwa kutumia nguvu ya ALMA, watafanya jitihada za kuutokomeza kwani jambo hilo linawezakana.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi, alisema changamoto kubwa iliyopo dawa za ugonjwa huokuuzwa bei kubwa hivyo zinapaswa kupungua chini ya dola moja ya Marekani.
Alisema Serikali ya ina mipango mizuri ya kutokomeza ugonjwa huo ambao unasabisha vifo visivyopungua milioni tatu barani Afrika wakati Tanzania wagonjwa ambao ni wanawake wajawazito na watoto hufikia 60,000 hadi 80,000 kwa mwaka
Mtendaji wa ALMA, Bi. Johannah-Joy Phumaphi, alisema taasisi hiyo ilianzishwa Septemba 2009 na viongozi wa Mataifa ya Afrika hadi sasa inawanachama 44.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment