19 July 2012
Mahakama yatupa pingamizi la Kakobe
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBC), Zakaria Kakobe dhidi ya wachungaji wa kanisa hilo waliomfungulia kesi ya ubadhirifu.
Kesi hiyo namba 79/2011, ilifunguliwa Mei 26, 2011 na wachungaji watatu wa kanisa hilo ambao ni Deuzidelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma.
Wachungaji hao wanamtuhumu Askofu Kakobe kwa ubadhirifu wa wa mali na pesa za kanisa hilo zaidi ya sh. bilioni 14 na ukiukwaji wa katiba ya kanisa hilo.
Hata hivyo, Askofu Kakobe kupitia Wakili wake Bi. Miriamu Majamba, aliweka pingamizi la awali akidai wachungaji hao hawana haki ya kisheria kumfungulia mashtaka kwani tayari walifukuzwa na Bodi ya Wadhamini wa kanisa hilo tangu mwaka 2010.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote ambazo ziliwasilishwa kwa maandishi, ilitupa pingamizi la Askofu Kakobe na kuwapa ushindi walalamikaji.
Katika uamuzi wake dhidi ya pingamizi la awali, uliotolewa Juia 16 na Jaji Agustine Shangwa anayesikiliza kesi hiyo, alisema hati ya madai ya walalamikaji inaonesha sababu za madai na wana haki kisheria ya kumfungulia mashtaka Askofu Kakobe.
Jaji Shangwa alisema anakubaliana na wakili wa walalamikaji, Bw. Barnaba Luguwa, kuwa hati ya madai ya walalamikaji inabainisha kiini cha sababu ambapo kinadharia ina madai ambayo walalamikaji watapaswa kuyathibitisha.
Alisema baadhi ya mambo ambayo walalamikaji watapaswa kuyathibitisha ni pamoja na mabilioni ya pesa za kanisa hilo ambayo
Askofu Kakobe anadaiwa kuyatumia kibadhirifu.
Mengine ni mahubiri ya uwongo kwa waumini wa kanisa hilo kuwa kama watafunga pamoja naye watajikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI na wanweza kuponywa kwa jina la Yesu anayemwabudu.
Jaji Shangwa alisema walalamikaji watapaswa kuthibitisha kwamba mahubiri hayo ya uwongo ni makosa. Madai mengine ni Askofu Kakobe kufungisha ndoa waumini wake bila kuwapatia vyeti ambapo kufanya hivyo ni kosa ambalo watapaswa kulipwa fidia au
mlalamikiwa kuadhibiwa.
Baada ya kutoa uamuzi huo, Jaji Shangwa alipanga shauri hilo kuendelea Agosti 6 mwaka huu kwa ajili ya hatua ya usuluhishi huku akiwataka wadau katika kesi hiyo kuwatafuta maaskofu wengine kutoka madhebu tofauti ili kutoa ushauri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment