05 July 2012

Makala kuwakabidhi bendera wanamichezo wa Olimpiki



Na Amina Athumani

NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makala kesho anatarajiwa kuwakabidhi bendera ya taifa wanamichezo watakaokwenda kuiwakilisha nchi kwenye michezo ya Olimpiki itakayoanza Julai 27, mwaka huu London Uingereza.


Wanamichezo ni Samson Ramadhan, Msenduki Mohamed, na  Faustin Mussa watakaokimbia mbio ndefu za marathon, Zakia mrisho atakaekimbia meta 5,000, Seleman Kidunda atakayepigana uzito wa kg 69 na Magdalena Moshi atakaeogelea mtindo huru meta 100.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid  alisema sherehe za kuagwa kwa timu hiyo zimeandaliwa na kampuni ya vinywaji vya Coca cola.

Alisema msafara mzima wa wanamichezo hao utakuwa na watu 12 akiwemo Hassan Jaruf ambaye ni mkuu wa msafara, Charles Nyange Utawala, Abdalah Makalla Mtibamaungo na Zakaria Gwandu, Remmy Ngabo na Sheha Ali ambao ni makocha.

Alisema timu hiyo inaondoka mapema kwa ajili  kupata mazoezi yatakayogharamiwa na kamati ya mashindano ya Olimpiki London chini ya mwenyekiti wake Sebastian Coe ambapo baadhi ya wanaimchezo kutoka nchi mbalimbali tayari wamewasili jijini London kwa kambi hiyo ya mazoezi ambayo itafanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Rais huyo alisema michezo hiyo itashirikisha jumla ya nchi 205 ambapo Tanzania ni mara ya saba sasa inashiriki michezo hiyo ya Olimpiki huku katika kipindi chote ikiwa haijapata medali katika michezo hiyo.

No comments:

Post a Comment