20 July 2012

Mafunzo, Tusker zashindwa kutambiana *Yanga kuivaa APR leo



Na Speciroza Joseph

TIMU za Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya jana zimeshindwa kufungana katika mfululizo wa mechi za michuano ya Kombe la Kagame katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10 jioni

Licha ya timu hizo za Kundi B kutoka suluhu katika mechi hiyo, Mafunzo imefanikiwa kupenya hatua ya robo fainali kutokana na kuwa na pointi mbili baada ya kutoka sare mechi mbili.

Katika mechi ya kwanza Mafunzo ilitoka sare na Azam FC, ambayo nayo imebakiwa na kibarua cha kukutana na Tusker michuano hiyo ambapo mshindi atatinga robo fainali.

Mechi hiyo ilipooza kipindi cha kwanza na kuwafanya watazamaji kukosa uhondo waliokuwa wanautegemea kutoka kwa timu hizo, ambapo dakika ya tatu Selemani Kassim wa Mafunzo alishindwa kuifungia timu yake baada ya kufumua shuti lililotoka nje.

Katika kipindi hicho Tusker, ilifanya shambulizi la nguvu langoni Mafunzo dakika 24 ambapo Dennis Makaisi, akiwa katika nafasi nzuri alishindwa kuifungia timu yake bao la kuongoza.

Dakika ya 36, Jerry Santo nusura aifungie Tusker bao baada ya kupiga shuti kali la mbali lililookolewa na kipa wa Mafunzo, Khalid Mohadhi.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kucheza kwa nguvu, ambapo Selemani Kassim wa Mafunzo alipiga shuti kali la mbali ambalo hata hivyo liligonga mwamba wa lango na kutoka nje.

Tusker ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Patrick Kagogo, Fredrick Onyango na Makaisi wakaingia Obadia Ndege, Peter Opiyo na David Makumbi wakati mafunzo alitoka Ally Othman Mmanga akaingia Bakari Shaban.

Katika mechi iliyopigwa mchana kwenye uwanja huo, Atletico iliibuguza timu ya El Salaam Wau mabao 5-0 na kuifanya kuyaaga mashindano hayo ikiwa imeshindiliwa mabao 19-0 katika mechi tatu ilizocheza.

Mechi ya kwanza, timu hiyo ya Sudan Kusini ilibugizwa mabao 7-0 na APR, Yanga nayo idunga mabao 7-1.

No comments:

Post a Comment