20 July 2012

Korogwe si shwari, bodaboda wachachamaa *Walitaka kuvamia kituo cha Polisi, Mbunge Majimarefu awatuliza


Na Yusuph Mussa, Korogwe

SIKU moja baada ya wananchi kuwachoma moto watu wawili wanaodhaniwa kuhusika na mauaji ya mwendesha pikipiki ya kubeba abiria 'bodaboda', Athuman Ramadhan (28), uchunguzi uliofanywa na Majira umebaini hali si shwari wilayani humo.


Baadhi ya wananchi wilayani humo, jana waliandamana hadi Kituo cha Polisi Korogwe ili kushinikisha watuhumiwe wengine wa mauaji hayo ambao wanashirikiwa kituoni hapo, watolewe na kuchomwa moto kama walivyofanya juzi.

Kijana huyo aliuawa Julai 13 mwaka huu, kwenye Kijiji cha Kwamzindawa, kilichopo Kata ya Mnyuzi wilayani hapa.

Mbali ya kushinikiza watu hao kutolewa, pia walitaka kujua kwanini polisi wamesababisha mauaji ya mkazi wa mji huo ambaye inadaiwa alipigwa risasi katika vurugu za juzi kutokana na taarifa walizopewa.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, mwanaharakati Bw. Ibrahim Abdillah ambaye alikuwepo kituoni hapo wakati vijana hao walipoandamana, alidai waendesha bodaboda walimtuma mwenzao mmoja kwenda Magunga kuthibitisha kifo hicho.

“Kuna watu walivumisha mwananchi aliyepigwa risasi ya kifua Bw. Shaban Omar (25), amefariki, lakini mwenzao alipofika Hospitali ya Magunga akakuta yupo hai lakini tayari vijana walijiandaa kuvamia kituo ambapo askari wanne wenye silaha walikuwa wamejipanga kuwakabili,” alisema Bw. Abdillah.

Mwendesha bodaboda (jina tunalo), alisema walijiandaa kuvamia kituo hicho ili kuwatoa watuhumiwa wengine wa mauaji ya mwenzao na kutaka ufafanuzi kwanini wahalifu wanalindwa.

“Tulifika kituoni ili kuwataka polisi watukabidhi watuhumiwa wa mauaji tukawachome moto kama wenzao, pia tulitaka kujua hali ya mwenzetu aliyepigwa risasi ya kifua baada ya kusikia amefariki dunia,” alisema mwendesha bodaboda huyo.

Mkuu wa Polisi wilayani hapa, Bw. Madaraka Majiga, alisema ni kweli vijana hao pamoja na wananchi wengine walifika karibu na kituo hicho ili kufuatilia taarifa za mauaji ya watu wawili ambao jana yake walichomwa moto.

“Hawakufika kituoni ili kuvamia, bali walitaka kujua nini kinaendelea baada ya mwenzao kuuawa,” alisema Bw. Majiga na kudai kuwa, hadi sasa hawajapata majina ya watu waliouawa zaidi ya mmoja kujulikana kama Rasta.

Kutokana na mauaji ya watu hao, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo, alisema wataunda Tume kuchunguza mauaji hayo na kupigwa risasi kwa wananchi.

“Katika tukio hili, huwezi kuacha lipite hivi hivi, nitaunda Tume ili kuchunguza, tumeshakubaliana tutakaa kikao cha pamoja na Kamanda wa Polisi mkoani hapa (Constantine Masawe), Julai 22 mwaka huu ili kujadili mustakabali wa usalama mjini hapa.

“Majeruhi waliopigwa risasi wapo saba ila watano tumekubaliana wapelekwe Hospitali ya Bombo ili wapate huduma ya matibabu ya haraka,” alisema.

Wananchi hao walipigwa risasi na polisi baada ya jitihada za kuwataka wawaachie watuhumiwa wa mauaji ya mwenzao kushindikana.

Awali polisi walipiga risasi hewani na mabomu ya machozi, lakini wananchi hao hawakutaka kuwaachia ambapo askari walipoona maisha yao yapo hatarini waliamua kufyatua risasi za moto ambazo ziliwajeruhi wananchi watano.

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani, maarufu 'Majimarefu', alidai kufanya kazi kubwa ya kuwahakikishia waendesha bodaboda kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha kwa kupigwa risasi pamoja na kuwashawishi vijana hao waondoke karibu na Kituo cha Polisi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Magunga, Dkt. Omar Sukari, alikiri kupokea majina ya watu saba waliojeruhiwa kwa risasi, ambapo kati ya hao, watano wamepelekwa Tanga, wengine wametibiwa na kuruhusiwa, askari waliojeruhiwa ni watatu.

2 comments:

  1. SIASA ZA UCHOCHEZI ZINAZOENDESHWA TANZANIA TUSIPOZIKEMEA YALIYOTOKEA TUNISI,LIBYA,MISRI NA SYRIA YANAKUJA MUDA MFUPI TENA SANA .KUUA NA KUBURUZA MAITI BARABARANI ALIFANYIWA ALIYEKUWA RAIS WA LIBERIA SAGENT SAMWEL DOE NI UNYAMA WA KUWEKWA KWENYE KUMBUKUMU INASIKITISHA DAMU YA UMWAGAJI DAMU BADO IKO AKILINI MWA VIJANA SASA TANZANIA NI JEHANAMU

    ReplyDelete
  2. NI VEMA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA PAMOJA NA KITUO CHA HAKI ZA BINADAMU WAWAJIBIKE IPO MIKANDA YA VIDEO INAYONESHA UNYAMA HUU ULIOKIDHIRI DUNIANI IWAPO WATUHUMIWA WALIOUAWA WATAKUWA HAWANA KOSA DAMU ILIYOMWAGIKA KOROGWE ITAKUWA LAANA KWA WAKAZI WA KOROGWE WOTE KWA UJUMLA SIO JAMBO LA KUFUMBIA MASIKIO NI VEMA UCHUNGUZI WA KINA UFANYIKE KURA ZA MAONI ZITUMIKE KUFICHUA WAHALIFU KOROGWE BADO ROHO YA KUUA WATUHUMIWA WA MAUAJI KOROGWE INAFUKUTA TUSIPOANGALI TUTASABABISHA MAUAJI YA KIMBARI KOROGWENI MJI UNAONGOZA KWA BADJAJ ,PIKIPIKI NA BAISKELI

    ReplyDelete