27 July 2012

Kizimbani kwa kutoa vyeti vya uuguzi, ukunga


Na Rehema Mohamed

MKAZI wa Tabata Bi. Veronica Danford (44), jana amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa makosa mawili ambayo ni kujivika utu na kutoa vyeti vya uuguzi na ukunga vyenye majina ya mtu mwingine.

Mbele ya Hakimu Faisal Kahamba, wakili wa serikali Bi. Wila Ahonga, alidai mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Februari 2007 hadi Mei 2012, ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Katika kosa la kwanza, ilidaiwa kwa makusudi na dhamira ya kufanya maovu, mshtakiwa alitoa cheti namba 18558 cha uuguzi akijifanya yeye ni muuguzi jambo ambalo halikuwa na ukweli.

Shtaka la pili ilidaiwa kwa nia ya udanganyifu, mshtakiwa huyo alijivika utu kwa kujifanya Bi. Lusia Kazohela na kutoa cheti cha ukunga chenye namba za usajili 13568, kuonesha kimetolewa kwake kama mkunga huku akijua si kweli.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa.

Akitoa masharti ya dhamna, Hakimu Kahamba alisema mshtakiwa  atakuwa nje kwa dhamana kama atakuwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya dhamana ya sh. 500,000 kila mmoja lakini
alishindwa kutimiza masharti hayo na kurudishwa rumande hadi Agosti 9 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, mshtakiwa huyo amezuiwa kusafiri nje ya Dar es Salaam bila ya kupata kibali cha mahakama hiyo.

No comments:

Post a Comment