16 July 2012

Kiini cha migogoro ya ardhi Handeni kinahitaji uchunguzi wa kina -CDCO


Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Maendeleo na Ushauri (CDCO), imewataka viongozi wa Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kiini cha migogoro ya ardhi wilayani humo.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo wa CDCO, Bw. Abraham Lukindo, amesema watendaji wa Serikali katika Idara ya Ardhi wilayani humo, wanachangia migogoro iliyopo kwa kuwadanganya viongozi.

Alisema umavimi wa mashamba wilayani humo kwa watu ambao wanayamiliki kihalali, unaonekana kushika kasi kutokaana na wahusika wa uvamizi huo kupata baraka za viongozi.

Alitolea mfano wa uvamizi wa shamba la umwagiliaji ambalo linamilikiwa na Umoja wa Makanisa, katika Kata ya Kwangwe, Kijiji cha Kwadoya, wilayani humo.

“Shamba hili linamilikiwa na Umoja wa Makanisa ambayo ni Anglikana, Kanisa Katoliki, Moramian, Lutheran, African Finland Church pamoja na taasisi za makanisa ambazo ni Christian Social Service Commission na Bugando Medical Centre chini ya Consultancy and Development Company Limited,” alisema.

Alisema CDCO inaamini kuwa, uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete kwa Bw. Muhingo Rweyemamu, kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo utasaidia kumaliza tatizo la uvamizi wa mashamba na migogoro ya ardhi kama atawajibika ipasavyo kutafuta kiini cha migogoro hiyo.

“Bw. Rweyemamu pamoja na viongozi wenzake wasikubali kudanyanywa, watafute kiini cha migogoro kwa kuzungumza na wamiliki halali wa mashamba yaliyovamiwa.

“Ofisa mmoja wa Serikali aliwahi kukiri kuhusika na mgogoro wa shamba letu na kusema makosa yameshafanyika, lakini bado aliwataka wananchi waandae muhtasari unaoonesha shamba letu wanalimiliki kihalali na walifanya hivyo usiku,” alisema.

Alisema umefika wakati wa Serikali kutokubali kuendelea kuhusishwa na migogoro ya ardhi inayotokana na watu ambao wanaomiliki mashamba kihalali kunyimwa hazi yao.

Bw. Lukindo alisema, uzembe wa kutoheshimu sheria za nchi na kutofuata maagizo ya Rais, kutaiweka Tanzania mahali pabaya na kuigeuza nchi sawa na Zimbabwe kutokana na migogoro iliyopo.

Alisema kauli ya Bw. Rweyemamu kutoa siku 14 kwa watu ambao wanaomiliki ardhi hekta 16,000 kujisalimisha kwake, hakiwezi kumaliza tatizo lililopo badala yake zitatochea fujo na uvamizi.

“Ni hatari kutoa kauli kama hii kwa sababu Serikali ina mpango wa kufufua mashamba yake yote ambayo yamekuwa yakilindwa na wananchi kwa kipindi kisichopungua miaka 20,” alisema.

No comments:

Post a Comment