19 July 2012

Katiba mpya ni suluhisho la matatizo ya watanzania?



Na Michael Sarungi

KWA kipindi kirefu sasa nchini kumekuwepo na mijadala mingi kuanzia kwa wasomi, wanaharakati na hata wananchi wa kawaida juu ya hatima ya nchi katika kimaendeleo.

Mengi yamesemwa juu ya kudumaa kiuchumi na wengine huku dawa ya kuondoka ikikosekana.


Maandalizi ya kuandikwa Katiba mpya, kubadilisha uongozi wa nchi kwa maana ya chama kingine kuingia madarakani, kupunguza madaraka ya Rais na mambo mengine ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele yanaweza kupunguza matatizo kwa kuleta ahueni kwa namna fulani lakini siyo jibu ya matatizo ya watanzania.

Hii ni kwa sababu Tanzania ya leo kila utakako kwenda ni matatizo hii ni kwa sababu asasi nyingi zilizotakiwa kuwa mstari wa mbele kutokomeza matatizo yanayowakabili watanzania pia ni sehemu ya matatizo.

Hapa namaanisha kuwa kuanzia kwa viongozi serikalini wa ngazi zote,  polisi, mahakama, idara ya mashtaka na nyingine ni uvundo mtupu.

Katika baadhi ya sehemu kubwa ya viongozi wamejijengea uchu wa kutaka kujitajirisha kwa kutumia jasho za wengine na kujikuta wakiweka kando kabisa miiko au viapo vya kazi zao.

Karibia viongozi wote katika maeneo hayo nyeti wamejihalalishia utamaduni wa chukua chako mapema kwani ule msamiati wa uzalendo kwao ni kama ndoto za mchana.

Riwaya ya James Hadley Chase 'The Guilty Are Always Afraid'  ikiwa na maana ya kuwa siku zote mtu muovu haishi kuwa na wasiwasi.

Nikiwa na maana kuwa, ili Tanzania ipige hatua ya kutoka tulipo hatuna budi kupata aina mpya ya viongozi kwa sababu hakuna kiongozi anayeweza kusimama na kweli akaonekana ni msafi kwa maana nyingine ni kuwa karibia viongozi wote waliopo wameshiriki kuifikisha nchi tulipo.

Kwa maana hiyo kila kiongozi anaona ni kama kujitia kitanzi mwenyewe kwa kuwa mstari wa mbele kutetea maslai ya wengi kwani akijiangalia yeye hana tofauti na mwenzake anaye tuhumiwa.

Kwa hiyo ili Tanzania itoke hapa inahitaji viongozi wapya, wema na waadilifu watakaoanzisha na kusimamia kiukweli harakati hizi zilizojengeka miongoni mwa viongozi wetu za kutowachukulia hatua wala rushwa na mafisadi papa.

Kama hiyo haitoshi tunahitaji viongozi wapya waadilifu kuanzia katika ngazi zote licha ya kupambana na utamaduni huu wa kulindana lakini pia watakuwa ni waadilifu katika suala zima la kuheshimu na kuziogopa fedha za umma.

Ukiitazama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ni nzuri wala haina matatizo makubwa kwa kiwango hicho licha ya matatizo madogo yaliyopo.

Tatizo kubwa lilopo nchini leo siyo Katiba, madaraka makubwa ya Rais na matatizo mengine bali ukosefu wa maadili au miiko ya uongozi kama ilivyo kuwa enzi za Azimio la Arusha.

Tanzania ya leo inakwenda kama meli iliyopoteza mwelekeo na nahodha ameshajitosa baharini kwa hiyo kila mmoja anaangalia ni jinsi gani atakavyoweza kujinasua kutokana na kifo kilicho mbele yake.

Tanzania ya leo baada ya viongozi kwa sababu zao binafsi wanazozijua kwa maslahi yao na marafiki wao, familia zao kuliondoa Azimio la Arusha imebaki kama shamba la bibi kila mtu mwenye nafasi anafanya kila analotaka.

Huu ni utamaduni wa hovyo ambao hauwezi kutufikisha kokote zaidi ya kuzidi kukuza kundi la watu wenye nacho na wasiokuwa nacho ambayo hatima yake ni milipuko kama mabomu ya mbagala.

Uandishi huo wa Katiba mpya utakuwa ni kazi bure endapa hatutarudisha miiko ya uongozi na wala katika hili wala tusidanganyane hakuna nchi yoyote duniani inayoendeshwa bila ya kuwa na miiko ya uongozi.

Ninachojaribu kueleza ni kuwa tusitarajie miujiza ya kupiga hatua kama hatutazirekebisha kasoro hizi zilizowasaidia viongozi wetu kuwa mabilionea kwa kipindi kifupi huu ni uvivu wa kufikiri.

Hapa ndipo tunapoona umuhimu wa kurejesha Azimio la Arusha na kuwa na viongozi watakaokuwa na nia thabiti ya kuisimamia miiko hiyo kama walivyokuwa watu kama Marehemu Edward Moringe Sokoine.

Au tuanzishe mfumo utakaoitwa 'Sokoine Part two' kuirejesha kazi  aliyoanzisha Marehemu Sokoine miaka ile ya 1980 vita hiyo iliyokuwa ikilenga kuwafichua wahujumu uchumi na wote tulishuhudia matokeo yake.

Tulishuhudia kwa kiasi kikubwa jinsi walanguzi na wahujumu uchumi wa miaka hiyo walivyoingia woga kiasi cha wengine kutupa pesa na bidhaa mbalimbali vilevile tukashuhudia kwa kiwango kikubwa jinsi woga ulivyowaingia mafisadi wa miaka hiyo.

Rejea (The guilty are always Afraid) tukawashuhudia hata wale walanguzi ambao iliaminika kuwa hawawezi kukamatika wakihaha kujiponya na kiama kilichokuwa mbele yao kiasi cha wengine kukimbia nchi.

Kwa vyovyote vile endapo tutafanikiwa kurejesha ile miiko ya uongozi na kuwa na utaratibu maalumu wa kuwashitaki wote waliohusika kwa njia moja au nyingine kuihujumu nchi yetu na kuifikisha ilipo na ikibidi hata kutaifisha mali zao hilo linaweza kuirudisha nchi yetu katika mstari ulionyooka kama ilivyo kuwa enzi za mwanzo.

Kama alivyo pata kunena hayati baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa ukitaka kuliongelea Azimio la Arusha sasa hivi inakulazimu kuwa na roho kama ya mwenda wazimu lakini iwe isiwe tutakuwa tunadanganyana tu kama hatutakuja na mbinu na mikakati ya maana hata huo uandishi wa katiba mpya ni kujidanganya na kutafuna pesa za wananchi bure.

Kurejeshwa kwa Azimio la Arusha na kuwa na viongozi madhubuti wenye uwezo wa kuzisimamia sheria za nchi ndiyo njia pekee inayoweza kuliokoa taifa hili kutokana na matatizo yanayotukabili lakini si kukimbilia huu uandishi wa katiba mpya.

Natoa wito kwa viongozi wetu wakae wakijua kuwa mwalimu ambaye wamekuwa wakimtukuza kinafiki alitumia Katiba hihi ambayo sasa hivi tunaiona kuwa ndiyo chanzo cha matatizo yetu.

Ni kweli sote tunajua kuwa Katiba ndiyo sheria ya msingi katika nchi yoyote ile lakini Katiba hata kama itakuwa ni nzuri kwa kiwango cha namna gani lakini ikakosa usimamizi ni kazi bure tatizo la Tanzania ni ukosefu wa maadili na wala si Katiba.

Bila kufanya hivyo tunaweza kujisifu kuwa tunapiga vita ufisadi ilhali rekodi yetu inatusuta na hatuna hata chembe ya uwezo wa kuyathibitisha hayo tunayoyaimba.

Na kwa hawa viongozi wetu, wafanyabiashara, jamaa zao marafiki wao na familia zao waliopata utajiri kwa njia ya kifisadi au wizi wakae wakijua kuwa salama yao ni kuirudisha mali hiyo na kutangulia jela

No comments:

Post a Comment