19 July 2012
Maandamano yanayoendelea nchini yanaikumbusha nini Mahakama?
Na Mwandishi Wetu
KUMEKUWA na migomo na maandamano nchini licha ya serikali kuyakemea ili kuzuia uvunjifu wa amani.
Wananchi wengi wamejiwekea imani potofu kuwa bila kugoma hawawezi kupata haki zao ama kutekelezewa wanayohitaji.
Hali hii kwa kiasi kikubwa imesababishwa mashaka kwa wapenda amani kwani inapotokea wengi wao hukaidi amri ya polisi ya kusitisha mkusanyiko wao.
Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilipiga marufuku maandamano ya madaktari yaliyopangwa kufanyika Julai 16, mwaka huu kushinikiza kuundwa tume huru ya kuchunguza kutekwa, kuteswa kwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dkt.Steven Ulimboka.
Katibu wa MAT, Dkt.Rodrick Kabangila alikaririwa akisema kuwa, maandamano hayo waliyoyaita ya amani yalitarajiwa kuwashirikisha madaktari kati ya 800 hadi 1,000 na akatoa wito kwa wananchi wenye mapenzi mema na taaluma hiyo, kushiriki wakiwa na vitambaa vyeupe.
Akasema, “Madaktari wamepokea taarifa za wenzao kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji, ikiwamo kufukuzwa katika makazi yao kwa kutumia Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kunyimwa chakula, posho na kuelezea kuwa vitendo hivyo ni vya unyanyasaji na uonevu dhidi ya taalamu na udaktari wenyewe.”
Kadhalika, Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam lilipiga marufuku maandamano hayo siku hiyo hiyo, yakiratibiwa na Jumuiya ya Kiislamu kulaani kile kilichoitwa mgomo wa madaktari unaosababisha adha, mateso na hata vifo katika jamii kwa wagonjwa kukosa huduma za tiba.
Hii ni kusema kwamba, kama Jeshi la Polisi lisingekuwa makini kuona mbali, basi kungekuwa na makundi mawili ya maandamano yenye jumbe na hisia zinazokinzana kabisa.
Ndiyo maana Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Bw.Suleman Kova alisema maandamano hayo hayapaswi kufanyika kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za ki usalama, baadhi ya madai ya madaktari kuwa yameshughulikiwa na serikali na hata hivyo kubwa zaidi, suala la mgogoro huo liko mahakamani hivyo, kulijadili kwa njia hiyo, ni sawa na kuingilia uhuru wa Mahakama.
Hitaji la makundi hayo kutaka kufanya maandamano tofauti linatoa fundisho gani kwa umma na hasa Mahakama?
Kwangu, nia hiyo ni funzo kwa Mahakama zetu nchini kuona umuhimu wa kuwahisha kesi mbalimbali zikiwamo za uchochezi na hata uhalifu mwingine ukiwamo wa kisiasa.
Umma unapenda kuona kesi zinatolewa hukumu haraka ili haki itendeke na pia, ionekane imetendeka maana haki inayocheleweshwa, ni kama haki iliyoporwa.
Mang’amuzi yangu hayalengi kuishinikiza Mahakama wala kuifundisha cha kufanya, bali kuikumbusha kuwa pale inapowezekana kuwahisha kesi, basi iepuke kuahirisha kesi bila sababu za msingi.
Kwamba, hilo likifanyika vyema, litaepusha hatari inayowakabili wananchi wengi ya kujikuta wanakosa subira na uvumilivu na hivyo, kuamua kujichukulia sheria mkononi kwa kuwahukumu watuhumiwa nje ya vyombo halali vya sheria (Mahakama).
Kadhalika, kucheleweshwa kwa kesi mbalimbali hususan kesi za uchochezi, kuona kimakosa kuwa ni vyema kutumia njia nyingine kusema wanachoanza kukiona ikiwa ni pamoja na kutaka kufanya maandamano na hata kutaka kutoa matamko na kujaribu kuibua mijadala katika maeneo mbalimbali rasmi, licha ya kujua kuwa suala hilo lipo katika mikono ya Mahakama.
Hao, ni wale wanaochukizwa na mambo mbalimbali yakiwamo matamshi, lugha na vitendo vya uchochezi vinavyohatarisha amani na usalama wa raia na mali zao katika nchi.
Kimsingi wanaofanya hivyo, ni pamoja na wanasiasa, wanafunzi katika taasisi mbalimbali za elimu kama vyuo na vyuo vikuu na wafanyakazi wa idara na sekta mbalimbali ikiwamo ya afya ambao sio siri, vitendo vyao vinachochea na kuhatarisha usalama wa nchi.
Ikumbukwe kuwa, nje ya mahakama, upo uwezekano mkubwa kwa watu kutuhumiwa tuhuma zisizo za kweli na wengine wakatuhumiwa kwa tuhuma za kweli hivyo ili kuondoa utata na kila upande kupata haki yake, ni vyema wahusika wakafikishwa mbele ya mahakama ili haki itendeke haraka haijalishi ni upande gani utaona uchungu au utamu.
Naiomba Mahakama izingatie ukweli kuwa, awe mlalamikaji au mlalamikiwa, hakuna kati yao anayepaswa kunyang’anywa wala kucheleweshewa haki yake, bali kuipata kwa wakati unaofaa maana upandacho, ndicho uvunacho.
Mahakama ikumbuke kuwa, nje ya Mahakama ni kusingiziana tupu; ni kuoneana na kudhulumiana na kubwa zaidi, nje ya Mahakama, kila mmoja anamhukumu mwingine kadiri anavyopenda yeye na hapo, ndipo kuna kukomoana, na hata kunyang’anyana haki.
Nchini, kumekuwa na tuhuma mbalimbali kuhusu watu wanaodaiwa kufanya uchochezi, maandamano na migomo isiyo halali na inayohatarisha usalama wa umma.
Hao kwa kutofikishwa mahakamani, usalama wao unakuwa mashakani maana jamii inawatazama kwa macho ya chuki.
Kadhalika, hatari hiyo inawakumba hata walio mbele ya Mahakama, lakini ikafanya kosa la kuchelewesha kesi zao wakiwamo wanaohatarisha usalama wa taifa kwa kutoa kauli za vitisho, uhaini na uchochezi katika maeneo mbalimbali yakiwamo majukwaa ya kisiasa na maeneo ya huduma zao kwa jamii.
Watumishi mbalimbali wakiwamo walimu na hasahasa madaktari, hawaachwi nyuma kwa kuzembea na hata kufanya migomo ya makusudi hali “inayoliua taifa” na kubwa zaidi, kuwaua wagonjwa waliostahili kupata huduma za tiba.
Kubwa zaidi, yamekuwapo madai mbalimbali miongoni mwa jamii kuwa hata migomo ya wataalamu wa afya ni masuala yanayopikwa, yakaandaliwa na hata kusimamiwa na watu wenye nia mbaya na taifa na kwamba, hao wamekuwa wakifanya ufadhili ili wahusika wakiwamo baadhi ya vinara wa migomo ikiwamo hii ya madaktari, waifanye nchi isitawalike kwa sababu zilizo sirini mwao.
Ndiyo maana, wachochezi wa mambo niliyoyataja nawaona kama watu wenye mkakati maalumu; tena wa kisiasa unaolenga kuona watu wanadhuriana, wanauana na hata kuifanya nchi ishindwe kutawalika ndani ya utawala bora wa kisheria.
Ni kama wanaiandaa nchi kumwaga damu jambo ambalo hakuna Mtanzania anayelihitaji wala kuomba litokee.
Matokeo ya haya yote, madhara kama vifo kwa wagonjwa kutokana na migomo ya madaktari na hofu kwa wananchi kutokana na kauli za uchochezi yanaongezeka na kuiathiri jamii kijamii, kiuchumi na hata kiafya na kisaikolojia.
Kwa msingi huo, ni wakati sahihi kwa Mahakama yetu, kuangalia uwezekano wa kuharakisha utoaji wa hukumu za kesi mbalimbali na hasa hasa, kesi za uhaini, kesi za uchochezi na kesi za mauaji kwa mtindo wowote yakiwamo mauaji kupitia migomo ya watoa huduma kama madaktari.
Ifahamike kuwa, kesi za namna hii ni hatari kucheleweshwa kuliko hata kesi za mambo ya uchaguzi hivyo, Mahakama isijikite kukuza demokrasia kwa kuendesha haraka kesi za uchaguzi, lakini ikasahau na kuwa na mwendo wa kinyonga kwa kesi nzito na nyeti kama zile zinazowahusu watuhumiwa wa uzembe na uchochezi unaosababisha mateso na vifo kwa wagonjwa ambao ni ndugu, jamaa, marafiki na majirani za watu.
Jamii inapenda kuona haki ikitendeka hivyo, nashindwa kujua kuwa waliofiwa au wanaoendelea kuteseka na wagonjwa kutokana na mgomo wa madaktari, wakitaka kuingia barabarani kulipiza kisasi kupitia sheria mkononi kwa watuhumiwa wao, tutawazuiaje.
Jeshi la Polisi linapofanya kazi yake ya kukamata watuhumiwa, kuwahoji na hatimaye kuwafikisha mahakamani, Mahakama itumie haraka wataalamu wake kutenda haki kwa pande zote yaani mlalamikaji na mlalamikiwa maana kutuhumiwa hakumaanishi kuwa umetenda kosa.
Ucheleweshaji kesi bila sababu za msingi ni hatari kwani wananchi wanaoshinda mahakamani kutafuta haki zao, wanapoteza muda mwingi ambao wangeutumia kuzalishaja mali na ni mateso makubwa kwao kisaikolojia.
Hivyo, Mahakama ikiwahisha kesi dhidi ya wachochezi, itasaidia kupunguza kasi ya kutisha ya jamii kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha haki kucheleweshwa mahakamani.
Kwa kasumba chafu ya kujichukulia sheria mikononi iliyojijenga miongoni mwa jamii, nalazimika kuamini kwamba huenda hao wanaojichukulia sheria mkononi, ndio waliomdhuru Dkt. Ulimboka.
Huenda waliomfanyia unyama huo ni mmoja wa viongozi muhimu wanaodaiwa kutuhumiwa katika mgomo wa madaktari, ni wale waliokuwa na kinyongo dhidi yake kutokana na kusimama kidete kuchochea mgomo huo hivyo, kuwafanya ndugu na hata wagonjwa wenyewe kupata mateso na maumivu makali, huku wengine wakifariki duniani kutokana na mgomo wa madaktari.
Ifahamike kuwa, uchochezi unapofanywa waziwazi na kisha kesi zake zikachelewesha, huwahamasisha wengine kuona kwamba sheria (Mahakama) zetu ni butu hivyo, wakadhani kuwa ni vyema na hakuna shida hata wao wakiiga mkumbo huku walioanza, wakiongeza kasi na matokeo yake, ndiyo hayo hata baadhi ya watu wanavifanyia kiburi cha wazi baadhi vyombo vya sheria na dola (Polisi).
Kimsingi kwa mfano, ni ajabu na inashangaza na hata kumfanya mtu ashindwe kujua huyu anajiamini nini kiasi kwamba asihofu wala kuheshimu agizo la Mahakama, mtu anajimini kiasi gani kiasi cha yeye kuamua kuitisha vyombo vya habari ili kutangaza kile alicho na taarifa zake za kutosha kuwa, kimekatazwa.
Ndiyo maana ninaiomba Mahakama iwahishe kesi ili wananchi wema, wasiingie katika hatari ya kushawishika kuingia barabarani kuwakumbusha wahusika (Mahakama) ili itimize wajibu wake mapema.
Jambo hili si jema na halitakiwi maana ni hatari.
Ninashauri kuwa, kesi za uchochezi na mgomo ziendeshwe haraka ili haki ipatikane haraka maana, kwa kiasi kikubwa jamii imechukizwa na migomo, maandamano na uchochezi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa taasisi, vikundi, taaluma au wanasiasa.
Watuhumiwa wa makosa ya uchochezi na uhaini nao watendewe haki inayopatikana mbele ya vyombo maalumu vya sheria (Mahakama) kama inavyofanyika kwa watuhumiwa wa wizi wa kuku.
Mahakama yetu itambue kuwa, kadri inavyoweza kuchelewesha suala hatari kama hili, ndivyo jamii inavyoweza kuendelea kupoteza imani na serikali na kuifanya ionekane ya hovyo na iliyolala usingizi wakati watu wameamka na wanaona kila mchezo unaochezwa.
Ndiyo maana najiuliza kuwa, maandamano tofauti yaliyokuwa yamepangwa kufanywa na madaktari na Jumuiya ya Waislamu, yanaikumbusha nini Mahakama?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment