10 July 2012

Francis Cheka kuwekwa kitimoto leo



Na Mwali Ibrahim

BAADA ya bondia Francis Cheka kukataa kupigana na Japhet Kaseba huku akiwa tayari anamkataba wa kupigana pambano hilo, waandaji wa pambano hilo wanatarajia kukutana leo pamoja na Cheka ili kuweza kujadili hatua ya kumchukulia.


Cheka alifanya kihoja hicho mbacho hakijawahi kutokea kwa bondia mkubwa kama yeye kwa kuingia ulingoni huku akiwa amevaa mavazi yake ya kawaida, ambapo mpinzani akiwa tayari kwa ajili ya pambano na kushuka bila kupigana.

Pambano hilo ni pambano lililokuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa ngumi nchini na ndio maana baada ya Cheka kufanya kihoja hicho walilazimika kumrushia makopo ya maji na kumzomea ambapo Kaseba alipewa ubingwa huo.

Siku moja kabla ya pambano hilo Cheka alisema hawezi kupigana na bondia asiyekuwa na kiwango kucheza naye ni sawa na kujishushia hadhi, kitu ambacho baadhi ya makocha wake walikipinga na kudai huo ni mchezo wa kirafiki ambao hauwezi kumpunguzia kitu na kumsihi acheze ambapo yeye alikana.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Promota wa pambano hilo Kaike Siraju alisema hakufurahishwa na kitendo hicho hata kidogo na yupo tayari kumchukulia hatua yoyote Cheka hata ikiwa kumfikisha mahakamani.

"Sikuwahi kutegemea Cheka kuyafanya mambo ya ajabu kama haya, niliyemzoea ni Maugo ambaye alikuwa akisema hachezi lakini siku ya pambano anapanda ulingoni lakini si kwa bondia mkubwa kama huyu kwa kweli alichokifanya sio kizuri," alisema.

Aliongeza kuwa kikao hicho cha leo kitamuhusisha yeye, Cheka, Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBC) na Oganizesheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBO) kuweza kulijadili hilo kwa pamoja na kuangalia hatua watakayomchukulia Cheka.

No comments:

Post a Comment