03 July 2012
Dkt. Shein kuzindua tamasha la ZIFF
Na Amina Athumani
RAIS wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, anatarajia kuzindua tamasha la 15 la filamu la nchi za majahazi, 'Zanzibar International Film Festival' (ZIFF), litakaloanza Julai 9 mwaka huu Ngome Kongwe Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Uhusiano wa ZIFF, Julueth Andy alisema pamoja na Rais Shein pia wapo wageni mbalimbali wakiwemo mabalozi na viongozi mbalimbali.
Alisema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika na kwamba wageni kutoka nchi mbalimbali wataanza kuwasili Julai 5, mwaka huu kwa ajili ya tamasha hilo ambalo litakwenda pamoja na makongamano yatakayoendeshwa na wataalamu wa uendashaji na uongozaji wa filamu barani Afrika.
Ofisa huyo alisema pia wasanii wa filamu wa Tanzania, watapata jukwaa la kuelezea umuhimu wao katika kazi hizo na nini kufanyike ili soko la filamu nchini liliweze kukua kimataifa.
Alisema jumla ya filam 105, zitaoneshwa kwenye tamasha hilo huku za hapa nchini zikipewa kipaumbele kwa kuandaliwa siku maalumu ya kuoneshwa tofauti na filamu za kigeni, ambazo zitakuwa zikioneshwa mchanganyiko.
Andy alisema tamasha hilo, pia litatoa nafasi kwa filamu mbalimbali zitakazooneshwa kuingia katika kinyang'anyiro cha Filamu bora, uigizaji bora, mtayarishaji bora pamoja na tuzo nyingine.
Tamasha hilo linatarajia kufikia kilele chake Julai 15 mwaka huu ambapo litasindikizwa na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wa kizazi kipya Nassib Abdul 'Diamond', AT, Barnaba, Shilole pamoja na vikundi vya wasanii kutoka Zanzibar.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment