02 July 2012
Serikali yazigeukia halmashauri 'zinazoua' michezo
Na John Gagarini, Kibaha
NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba, Anjelina Kairuki amesema Kamati ya Bunge ya sheria itafuatilia halmashauri ambazo zitashindwa kutekeleza agizo la serikali la kutenga bajeti za michezo.
Aliyasema hayo juzi wakati akifunga mashindano ya 34 ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Shule za Sekondari (UMISSETA) kwenye Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha, Pwani.
Alisema serikali imekuwa ikitoa maelekezo kwa halmashauri kuweka mipango na kupanga bajeti kwa ajili ya kuendeleza michezo hasa ya vijana wadogo lakini utekelezaji imekuwa ni tatizo.
“Kamati ya sheria na katiba ipo hivyo tungependa yale yanayopendekezwa yafanywe kwa vitendo kwani tunaweza kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kupitia michezo,” alisema Kairuki.
Alisema ili nchi iweze kufanikiwa kimichezo ni lazima iwekeze kwa vijana kwenye michezo kwa gharama yoyote kwani kizuri ni gharama.
“Halmashauri zinapaswa kuhakikisha walimu wanapelekwa kwenye vyuo vya michezo na wanatumiwa ipasavyo na kuwe na viwanja vyenye ubora ili kuinua michezo nchini,” alisema Kairuki.
Aliwataka wazazi kutowakatisha tamaa watoto wao ambao wana vipaji vya michezo bali wawaunge mkono ili waweze kufikia mafanikio yao na nchi kwa ujumla
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment