11 July 2012

Bilal: Baadhi ya vyama vya siasa vinachangia matakaba


Na Peter Mwenda

ASILIMIA kubwa ya vyama vya siasa barani Afrika, vimejiondoa katika jukumu la kuboresha maisha ya wananchi badala yake vinaporomosha utu na kukuza matabaka kwenye jamii.

Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa vyama vya siasa vilivyopo madarakani na vyama pinzani kutoka nchi 11 barani Afrika.


Alisema baadhi ya vyama vya siasa havitekelezi kile wanachohubiri kwa wananchi hivyo kuichanganya jamii lakini katika nchi zenye Serikali makini, vyama vya aina hiyo vimethibitiwa.

“Madhara ya vyama vya siasa kuyakimbia matakwa ya jamii ni mengi, kubwa zaidi ni kupungua kwa idadi ya wapiga kura katika chaguzi mbalimbali na mengine yanaifanya jamii kuchukia kundi la wanasiasa kutokana na tabia yao ya kuzungumza mambo ya uongo ili kupata kura,” alisema Dkt. Bilal.

Aliongeza kuwa, eneo kubwa linalofanya vyama vya siasa vishindwe kufanya kazi zake vizuri ni ukosefu wa vyanzo vya mapato ambapo fedha inayoingia katika vyama hivyo kutokana na vyanzo mbalimbali inaleta matatizo kwa viongozi wa siasa katika maeneo mengi duniani.

Dkt. Bilal alisema, Tanzania imeweka sheria ya kuratibu fedha katika vyama vya siasa wakati wa uchaguzi lakini inahitaji washirika wote kuitekeleza kwa vitendo badala ya maneno.

“Tume ya kurekebisha katiba nchini, inafanya kazi ya kukusanya maoni katika maeneo mbalimbali na vyama vya siasa ni washirika wakubwa wa kuhamasisha wananchi watoe maoni yao badala ya kupandikiza mawazo na agenda za vyama,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa Taasisi ya Demokrasia nchini (TCD), Bw. James Mbatia, alisema tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi nchini, Serikali ambayo awali iliona ni uasi imebadilika na kuona matunda ya vyama vingi.

Alisema mtazamo wa vyama vya siasa ni kujenga demokrasia na kusaidia jamii kujua haki zao za msingi na njia wanayotakiwa kufuata kupata haki zao katika ngazi zote za uongozi.

Nchi zilizohudhuria mkutano huo wa siku tano ni Tanzania, Malawi, Msumbiji, Uganda, Tunisia, Kenya, Sudani Kusini, Zimbabwe, Burundi, Ghana na Mali.

No comments:

Post a Comment