19 June 2012

Yanga yaingia msituni rasmi *Berko, Asamoah wanogesha mazoezi


Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya Yanga, imeanza rasmi mazoezi jana kwenye Uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam ikiwa na wachezaji tisa wakiwemo kipa Yaw Berko na Keneth Asamoah huku kiungo wao mpya, Nizar Khalfan akiwa jukwaani akiangalia.

Gazeti hili lilifika Makao Makuu ya klabu hiyo, Mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam jana saa tatu asubuhi na kuikuta timu hiyo ikiendelea na mazoezi huku mashabiki wachache wa timu hiyo walijitokeza kuiangalia.

Wachezaji waliokuwepo katika mazoezi hayo yaliyokuwa chini ya Kocha Msaidizi, Fredy Felix 'Minziro' ni Berko, Oscar Joshua, Asamoah, Jeryson Tegete, Athuman Idd 'Chuji', Omega Seme, Ibrahim Job, Idrisa Rajab na Godfrey Taita.

Mazoezi hayo yaliendelea mpaka saa nne na nusu ambapo baada ya kumaliza wachezaji walisoma dua ya pamoja na kwenda kwenye vyumba vyao, huku mashabiki wakionekana kufurahishwa na kitendo hicho.

Gumzo lilikuwa kwa wachezaji Asamoah na Berko ambao waliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari kwamba wangeachwa na kufanya kuwepo makundi ya mashabiki kutumia muda mwingi kuwazungumzia, huku kila mmoja akishindwa kuelewa juu ya uwepo wa wachezaji hao.

Pia Nizar naye alikuwa kivutio licha ya kwamba hakufanya mazoezi kutokana na kuwa na udhuru, alikuwa akizongwa na mashabiki hao na kuamua kukaa mbali na wachezaji wenzake walipokuwa uwanjani.

Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Minziro alizungumza na gazeti hili na kusema kwamba timu yake imeanza mazoezi kwa ajili ya Ligi Kuu na Kombe la Kagame na kwamba wachezaji wengine wataendelea kuwasili.

Alisema ana imani kwa usajili walioufanya watatetea ubingwa wao wa Kagame pamoja na Ligi Kuu, hivyo amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwapa ushirikiano wachezaji wapya waliosajiliwa.

Akizungumzia kuhusu suala lake la kulipwa mshahara, Minziro alisema ameshamalizana na uongozi wa Yanga na kwamba kila kitu kinakwenda vizuri.

No comments:

Post a Comment