19 June 2012
Poulsen: Tumeshindwa kiume *Watanzania wa Maputo waipa 5 Stars
Na Mwandishi Maalumu, Maputo
KOCHA wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen amesema baada ya kupoteza mechi dhidi ya Msumbiji 'The Mambas', sasa atajipanga upya kwa ajili ya mashindano yajayo kwani timu yake imeonesha uwezo mkubwa katika mechi hiyo ya juzi.
Kim aliishuhudia Taifa Stars, ambayo kwa sasa inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ikiondolewa na Msumbiji kwa penalti 6-7 baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare bao 1-1 kwenye mchezo huo wa kusaka kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kim alisema Stars walicheza vizuri lakini wapinzani wao walitumia nafasi nzuri ya kuwa nyumbani na kushinda.
"Nawapongeza kwa kushinda, lakini najivunia vijana wangu kwa jinsi walivyoweza kucheza kwa umakini muda wote wa mchezo.
"Nilijua Msumbiji wangeshambulia kwa nguvu, lakini na sisi tuliweza kucheza soka yetu ya kawaida na kutegeneza nafasi nyingi, nashukuru tumeweza kusawazisha lakini katika penalti lolote linaweza kutokea.
Naye kocha wa Msumbiji, Gert Engels aliwasifu Stars kwa kucheza vizuri huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kushinda mchezo huo.
"Tanzania ni timu nzuri inacheza kwa uwelewano mkubwa, lakini wakati wa mapumziko niliwaambia wachezaji wangu watulie na wacheze kama nilivyoowaagiza.
Wanapaswa kuitunza hii timu ya Taifa Stars kwa sababu ina wachezaji wengi chipukizi wenye vipaji vya hali ya juu ni bahati mbaya tu tumewafunga kwenye penalti.
Naye beki Erasto Nyoni, alisema wamepokea kwa masikitiko matokeo hayo lakini aliahidi kuisaidia timu hiyo kwenye michezo mingine.
"Tunatakiwa kujipanga upya kwa ajili ya mechi za kusaka tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014, lazima tukubali matokeo," alisema Nyoni.
Naye nahodha msaidizi wa Stars, Aggrey Morris alisema hawana kingine zaidi ya kujiuliza wapi walipokosea, ili kurekebisha makosa hayo.
Watanzania wengi waliojitokeza kushuhudia mchezo huo walioneshwa kufurahhishwa na kiwango cha Stars na kusema hata kama wameondolewa, walicheza kwa kujituma.
Anuary Aziz, ambaye anafanya kazi Maputo alisema hajawahi kuona Watanzania wanaoishi nchini hapa wakijitokeza hivyo kushangilia timu yao na kuongeza kuwa walishapata taarifa kuwa Taifa Stars imeboreshwa.
“Kwa kweli timu imebadilika na kocha huyu asisumbuliwe aachwe afanye kazi yake, tumeshindwa lakini vijana wamecheza hadi dakika ya mwisho kwa kweli tumefurahi na tumeshangilia sana.
“Tanzania tutafika mbali sana tuwe na subira tu kwani wachezaji wetu wanatupa matumaini sana…mchezo huu ulikuwa wa kwetu lakini tumeshindwa kwa penalti tumekubali matokeo na tunajua tutafika mbali,” alisema Mohamed Ali ambaye ni Mtanzania mwingine anayeishi Maputo.
Stars inategemewa kuwasili leo usiku ikitokea Maputo kupitia Nairobi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment