05 June 2012

Wazee wamvaa Mosha agombee Yanga "Mwenyewe agoma, ahaidi kuwasaidia Kagame



Na Elizabeth Mayemba

ALIYEKUWA Makamu  Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Davis Mosha amesema kwamba hayupo tayari kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya klabu hiyo katika uchaguzi mdogo wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Julai 15, mwaka huu.


Mosha alitoa kauli hiyo wakati Wazee wa muafaka wa klabu hiyo wakiongozwa Katibu wake Ibrahim Akilimali walipoenda kumpa pole baada ya Alhamisi kufiwa na baba mkwe wake mzee Malick Said Kiongoli, ambapo pia walitumia fursa hiyo kumshauri mpiganaji huyo ili agombee nafasi moja wapo katika uchaguzi huo.

"Kwanza kabisa nawashukuru sana wazee wangu kwa kuja kunifariji katika kipindi hiki kigumu cha kufiwa na baba mkwe wangu Mzee Malick, na ombi lenu la kutaka nirudi kuiongoza Yanga nimelisikia lakini sitakuwa tayari kufanya hivyo,ila naomba niwaahidi kitu kimoja kuwa mimi ni mwanachama wa Yanga na mwenye mapenzi ya dhati na timu hiyo, nitakuwa tayari kutoa msaada wowote kwa timu hata kama nitakuwa nje ya uongozi," alisema Mosha

Alisema anashukuru kwamba wazee hao wametumia busara na hekima kubwa kwani tangu ajiuzulu wadhifa huo hakuwahi kukutananao, lakini juzi ndiyo kwanza amewaona hivyo hapuuziii ombi lao lakini kwa sasa hatakuwa tayari kuongoza Yanga lakini atakuwa bega kwa bega na timu hiyo.

Mosha alisema kuwa sasa timu hiyo inakabiliwa na michuano ya kombe la Kagame anachoahidi kwa wazee hao ni kushirikiana nao na kuhakikisha timu yao itatetea ubingwa wake ikiwa na kusajili wachezaji bora ambao watawaletea ubingwa.

Pia amewataka wanachama wa klabu hiyo kuwa makini katika kuchagua viongozi, wawachague wale ambao wanamapenzi mema na klabu na pia wenye uwezo kifedha na si wale ambao watataka kuja Yanga ili wanufaike na mapato ya milangoni.

"Chagueni viongozi ambao angalau watakuwa wanauwezo kifedha na hata kiuongozi, sio wale viongozi ambao wanategemea kujiendesha kupitia fedha za Yanga," alisema

Naye Mzee Ibrahim Akilimali alisema kuwa wanatambua kuwa Mosha ni mpiganaji kwani baada ya kujiuzulu alihakikisha anaisaidia timu hiyo na hatimaye ilitwaa ubingwa wa bara msimu uliopita, na ndio maana waaona watumie nafasi hiyo kumshawishi arudi tena Yanga.

"Hakuna ambaye hajui kuwa Mosha ni mpiganaji kila mwanayanga anajua hilo na ndio maana tukatumia fursa hii ili kumshawishi agombee, lakini ilimradi ametuahidi kuendelea kutusaidia hilo tunampongeza sana na sisi tunamuombea kwa Mungu afanikiwe hilo," alisema Akilimali.

No comments:

Post a Comment