01 June 2012

Wauguzi Kyela waaswa kutoa matibabu bure kwa wazee


Na Israel Mwaisaka, Mbeya

SERIKALI ya wilayani ya Kyela Mkoa wa Mbeya imesema haitawavumilia waganga na wauguzi watakaoshindwa kutoa huduma sahihi kwa wazee kufuatia tamko la Waziri Mkuu la kutaka wazee wote nchini watibiwe bure.

Katibu Tawala wa wilaya hiyo Bw. John Komba aliyasema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela Bi. Magreth Malenga kwenye mkutano maalumu uliowashirikisha waganga na wauguzi wafawidhi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Mkutano huo ulioandaliwa na Asasi ya SWOLO ili kuweza kuzungumza kwa pamoja na kujua nini tatizo la Wazee kushindwa kupata matibabu bila malipo wakati
serikali ilishatoa tamko.

Baada ya mkutano huo, alisema hatarajii tena kusikia malalamiko kutoka kwa wazee juu ya kutopata matibabu kwa sababu hawana pesa na kuwa kama kuna mtumishi wa afya anaona hawezi kutoa huduma kwa wazee bure, kama sera inavyoeleza ni bora akaiacha kazi hiyo ili wabaki waganga na wauguzi watakaoitekeleza sera hiyo ya serikali.

"Sioni sababu ya mtumishi wa afya kununa kwa sababu mzee anapewa huduma bure, kwani hiyo ni haki yake na dawa ni za Serikali wala siyo zake, sasa kama wapo watumishi wa aina hiyo basi watupishe kabla hawajachukuliwa hatua kali za kisheria," alisema.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya Bw. Festo Ndugange alisisitiza
kuwa huduma bure kwa wazee ni utaratibu uliowekwa na Serikali, hivyo ni lazima watumishi hao wa afya kuona wazee kupata huduma bila malipo ni haki yao.

Alisema, ofisi yake ilishatoa waraka kwenda katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zote juu ya agizo hilo na kusema kama kuna mtumishi anakwenda kinyume na agizo hilo hatavumiliwa kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kazi.

Alifafanua kuwa, wazee wamelitumikia taifa hili kwa muda mrefu na baadhi ya matunda wanayofaidi wauguzi yametokana na wazee hao, hivyo ni lazima wakaenziwa kama Serikali yenyewe ilivyowatambua.

Mkurugenzi wa Shirika la SWOLO linalojishughulisha na utetezi kwa wazee mkoani Mbeya Bw. Abel Ambakisye alisema lengo la kuitisha mkutano huo ni kutaka kuweka maazimio ya pamoja kuhusu matibabu ya wazee bila malipo ikiwa ni pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo na namna ya kuzitatua.

2 comments:

  1. TUACHE KUDANGANYA WATANZANIA KUWAAHIDI MAMBO YASIYOTEKELEKA NI VILE HATAKUWA WAMEBAKIA HATA HAO WAZEE WATAKUWA WAMEBAKIA WACHACHE WAKATI WA UCHAGUZI . KAMA SIKOSEI NILISIKIA SEIF SHARIF HAMAD AKIAHIDI USAFIRI BURE KWA WAZEE UNGEKUWA WAKATI MUAFAA KUONYESHA NJIA AKIWA MAKAMU WA RAIS ILIAKIWA ATAKAPOGOMBEA URAIS ASIWEKEWE MIZENGWE NI VEMA KUFANYA SENSA YA WAZEE ILI TUPANGE BUDGET YAO BILA KUTUMIA SIASA KUPANGA MAMBO YA KITAALAMU

    ReplyDelete