19 June 2012

Wasanii waipongeza bajeti ya serikali


Na Zourha Malisa

SIKU chache baada ya serikali kuwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013, bungeni mjini Dodoma, baadhi ya wasanii wameipongeza kwa kuweza kutambua mchango wa kazi zao kwa kuwaingiza katika mfumo rasmi utakaolinda kazi zao.


Wasanii hao wameipongeza serikali kwa jitihada za kuinua uchumi wa nchi na kipato cha msanii kwa kulinda kazi za wasanii kupitia mapato yatakayopatikana.

Akizungumza Dar es Salaam jana Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba alisema mfumo wa sekta rasmi utapunguza wizi wa kazi za wasanii pamoja na kulinda haki ya msanii.

“Kutakuwa na takwimu sahihi za mauzo ya kazi za wasanii na mapato ya wasanii, pia yataeleweka na mwisho wa mwaka unaweza kujua nani ameuza kwa kiwango gani,” alisema.

Alisema watakuwa na kila sababu ya kudai serikalini kwani kila kitu kitakuwa kipo wazi hivyo serikali itoe elimu kwa jamii, ili kujua kazi ipi ni sahihi kununua kwa ajili ya kuongezea pato la taifa.

Aliongezea kwamba wanyonyaji wanauchukia mfumo huo, kwani walishazoea kuwakandamiza wasanii hivyo mfumo huu ni tiba kwa wale wote waliozoea kujinufaisha kwa kupitia nguvu za wasanii.

No comments:

Post a Comment