14 June 2012

Waandishi, wachapishaji kufaidika na kazi zao


Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Muungano wa Vyama vya Wazalishaji na Wachapishaji Maarifa (KOPITAN), Bw. Abdullah Saiwaad, amesema kanuni na muongozo wa tozo kwa kazi zinazorudiwa utasaidia kuliongozea Taifa mapato.


Bw. Saiwaad aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika warsha ya siku moja kuhusu kanuni ya urudufishaji na hakimiliki na kusisitiza kuwa, kanuni hizo zitawasaidia waandishi na wachapishaji wa kazi za maandishi.

“Kanuni hizi zitasaidia ukusanyaji wa kodi kwa Taifa na wenye hakimiliki kunufaika kutokana na kazi zao ambazo muda mrefu zimekuwa zinarudufiwa kinyume na sheria,” alisema.

Katika warsha hiyo, njia mbalimbali za ukusanyaji mapato za kurudufu kazi zenye hakimiliki zilielezwa pamoja na namna ya kutekeleza mifumo hiyo.

Mifumo ya ukusanyaji mirabaha kwa kiasi kikubwa imeletwa ili  kulinda na kuzipa hadhi kazi za wazalishaji ambao ni waandishi na wachapaji mbalimbali.

Aliongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa wimbi kubwa la kurudufu kazi za sanaa, Chama cha Hatimiliki nchini COSOTA kinashirikiana beka kwa bega na KOPITAN kuhakikisha mfumo na muongozo wa kanuni hizo ambazo Serikali inatarajia kuzitoa, utakuwa daraja bora la mafanikio ya kuhakikisha kazi za wasanii na waandishi zinalindwa ipasavyo.

“Tuna nia ya kuwa na mfumo bora ambao kila mtu atanufaika, kuja kwa mfumo huu ni mafanikio bora ambayo yatanufaisha watu wote,” alisema Ofisa Mtendaji wa COSOTA, Bw. Yustus Mkinga.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afrika wa Shirikisho la Kimataifa la Haki za Urudufishaji (IFRRO), Bw. Greenfield Chilongo, aliwataka wamiliki wa haki za kazi mbalimbali za kimaandishi na sanaa nyinginezo, kusimamia haki za umiliki wa kazi zao ili kuzuia urudufishaji wa kazi hizo unaofanyika bila kufuata sheria na kanuni za hakimiliki.

No comments:

Post a Comment