19 June 2012
Uchaguzi Yanga waingia 'gundu' *Wagombea wote wawekewa pingamizi
Na Mwandishi Wetu
UCHAGUZI wa Yanga, uliopangwa kufanyika Julai 15 mwaka huu umeingia 'gundu' baada ya aliyewahi kuwa Mhazini wa klabu hiyo Ahmed Falcon kuwawekea pingamizi wagombea wote.
Akizungumza Dar es Salaam jana Falcon alisema ameamua kuweka pingamizi kutokana na kwamba uchaguzi unafanyika na katiba ambayo haijasajiliwa na Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo.
"Nimeamua kuwawekea pingamizi wanaowania uongozi Yanga kwa kuwa wanafanya uchaguzi usio halali kuwa katiba wanayotumia bado haijasajiliwa na msajili," alisema.
Alisema yeye kama mwanachama halali wa Yanga, hawezi kuona taratibu zinakiukwa baadhi ya watu kutokana na maslahi yao binafsi.
Falcon ambaye alijiuzulu Yanga, wakati wa uongozi wa Imani Madega alisema huu si wakati wa kufumbia macho madudu yanayotaka kufanywa na wasioitakia klabu hiyo mema.
Alisema atahakikisha anafuatilia maslahi ya Yanga hadi kieleweke kwa kuwa kukaa kimya ni kuitakia mabaya klabu hiyo kongwe.
"Ni lazima tuwe na uchungu na klabu yetu, hatuwezi kuona kanuni na taratibu zinavunjwa makusudi kwa kuwa ilitakiwa kuisajili katiba kama ilivyo kwa vyama vingine," alisema.
Baadhi ya wanachama waliojitokeza kuwania uongozi wa klabu hiyo ni pamoja na aliyewahi kuwa mdhamini Yusuf Manji, John Jambele na Sarah Ramadhan wanaowania nafasi ya Mwenyekiti.
Wagombea wengine waliojitokeza ni Yono Kevela, Ayoub Nyenzi, Ally Mayay na Clement Sanga wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment