19 June 2012

Stars yatolewa kwa mbinde AFCON


Na Mwandishi Wetu, Maputo

TIMU ya Taifa (Kili Taifa Stars), jana imetolewa kiume na Msumbiji 'Mambas' katika mechi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Katika mechi hiyo Taifa Stars ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 7-6, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida. Katika hatua hiyo ililazimika kupigiana penalti zaidi ya tano baada ya kila timu kufunga mikwaju yote.


Mechi hiyo ilipigwa katika Uwanja wa Taifa wa Zampeto jijini Maputo.

Katika mechi hiyo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 dakika 90 za kawaida na kulazimika kutumika sheria za kupigia penalti ambapo washindi waliibuka na mabao 7-6.

Awali timu hizo ambazo zilikutana jijini Dar es Salaam, mwanzoni mwa mwaka huu zilitoka sare sare ya bao 1-1.

Katika mechi hiyo Stars ndiyo iliyoanza kufungwa kipindi cha kwanza kwa bao lililofungwa na Jeremies Saito aliyeunganisha krosi ya Helder Pelembe.

Kipindi cha pili Stars iliingia kwa nguvu na kutandaza soka la uhakika kwa lengo la kutafuta mabao, lakini ukuta wa wapinzani wao ulikuwa mgumu kupitika kutokana na mabeki wake kuwa imara.

Juhudi za vijana hao wa Poulsen zilizaa matunda dakika ya 90, baada ya kupata bao lililofungwa na Agrey Morris baada ya kuunganisha kona iliyochongwa na Amir Maftah.

Baada ya dakika 90 kumalizika ndipo sheria za mikwaju ya penalti ikatumika ambapo wachezaji wa Stars Mbwana Samatta, Morris na Kelvin Yondani walikosa na kuifanya Msumbiji kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment