15 June 2012
Timu za Mbeya zatinga nusu fainali
Na Mwandishi Wetu
TIMU za soka za Mkoa wa Mbeya za wanaume na wanawake zimejihakikishia kucheza nusu fainali ya michuano ya kukuza vipaji wenye umri chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars inayotarajiwa kuanza leo kwenye Uwanja wa Karume, Jijini, Dar es salaam.
Timu hizo zimefuzu kucheza nusu fainali hiyo baada ya kumaliza katika makundi yao zikiwa zinaongoza.
Nayo Arusha imefanikiwa kupitisha timu zake zote za wanaume na wanawake baada ya kushika nafasi ya pili katika kundi A nyuma ya Mbeya.
Mbali na timu hizo, zingine zilizofuzu kwa upande wa wanaume ni Temeke ilioonesha kuwa tishio katika michuano hiyo kwa kufunga idadi kubwa ya mabao.
Ilianza kwa kuisambaratisha Lindi kwa mabao 12-2 kabla ya kuichakaza tena Ilala kwa mabao 3-0. Wakati wanaume wamefuzu, timu yao ya wanawake inasubiri matokeo kati ya Ilala na Lindi zilizotarajiwa kucheza jana.
Hata hivyo, kwa upande wa wanaume timu ya mwisho itakayoungana na timu hizo inategemea matokeo ya mechi za mwisho za makundi zilizotarajiwa kuchezwa baadaye jana, sambamba na kwa upnade wa wanawake.
Katika mechi zilizochezwa juzi asubuhi timu ya wanawake ya Temeke iliichapa Ilala kwa mabao 2-0.
Kwa upande wa wanaume, Temeke iliendeleza mwendo wake wa kugawa dozi baada ya kuibugiza Ilala kwa mabao 3-0. Goli la kwanza la washindi lilifungwa na Khalid Mwenda dakika ya 28, la pili liliwekwa kimiani na Paulo Balama dakika ya 43 na la mwisho lilpatikana dakika ya 87 kupitia kwa mshambuliaji wake hatari, Bakari Ally.
Katika mechi nyingine iliyochezwa jioni, timu ya wanawake ya Arusha iliifunga Kinondoni kwa mabao 2-0, kupitia kwa Anitha Antony dakika za pili na 35. Mechi ya mwisho ilizikutanisha Kinondoni na Arusha ambapo zilitoka sare ya mabao 2-2. Wafungaji wa Arusha ni Nazir Abdul dakika za 22 na 82, wakati yale ya Kinondoni yaliwekwa kimiani na Omar Ramadhani na Jarufu Lutonga katika dakika ya 55
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment