15 June 2012
Tuzo za filamu za kibongo kufanyika Julai
Na Zahoro Mlanzi
KAMPUNI ya Bantu inatarajia kuandaa tamasha la utoaji tuzo za filamu nchini (Bantu Film Awards), litakalofanyika kwa mara ya kwanza Julai jijini Dar es Salaam likiwa na lengo la kutambua kazi za wasanii na kuzitangaza kimataifa.
Akizungumzia tamasha hilo Dar es Salaam jana, Ofisa wa kampuni hiyo, Stewart Kambona alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na kwamba wapo katika mazungumzo na wadau mbalimbali wa sanaa, wakiwemo waadhiri wa vituo vya sanaa kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Alisema tamasha hilo linatarajiwa kufanyika mwezi ujao Dar es Salaam, ambalo litasaidia kutoa motisha kwa wasanii wanaochipukia na hata wale wakongwe katika fani hiyo kuongeza bidii katika kuandaa kazi zao.
"Unajua hili tamasha litakuwa ni chachu ya wasanii kuzidi kupata mafanikio kwani wakiona mwenzao leo amepewa tuzo kutokana na kazi yake fulani, nina hakika atajipanga ili mwakani naye apewe tuzo, tunatarajia tuzo hizi kufanyika kila mwaka," alisema Kambona.
Alisema kwa kuanzia kutakuwa na kategoria 27 ambazo alizitaja baadhi yake kuwa ni tuzo ya muongozaji bora, mtunzi na mpiga picha ambapo watahakikisha wanatoa fursa kwa wadau kutoa michango yao, ili kusiwepo na maneno ya hapa na pale baada ya kutoa tuzo hizo.
Naye Wasanii Jacob Stephen 'JB' na Irene Uwoya wakizungumza kwa niaba ya wasanii wenzao kwa nyakati tofauti, waliishukuru kampuni hiyo kwa kuwa na wazo hilo ambalo wanaamini litasaidia kuinua tasnia ya filamu hapa nchini ndani na nje ya nchi.
JB alisema wamekuwa wakifanya sanaa kwa muda mrefu, lakini hakukuwa na kitu cha kuwatia moyo ila hivi sasa kila mmoja ataongeza ubunifu wake katika kuandaa kazi ili mwisho wa mwaka wapate tuzo.
Naye Uwoya alisema tuzo hizo kwao ni changamoto ya kuzidi kufanya vitu vizuri zaidi, kwani ana imani tuzo hizo zitawatambulisha kimataifa kupitia kazi zao na mwisho wa siku mafanikio ya fani hiyo yataongezeka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment