01 June 2012

TASAF wazijengea Kaya 2,331 uwezo



Na John Gagarini, Kibaha

JUMLA ya kaya 2,331 zinazoishi kwenye mazingira magumu wilayani Kibaha
Mkoa wa Pwani zimenufaika na Mpango wa Uhawilishaji Fedha kwa kaya hizo
kwa kupatiwa kiasi cha sh. milioni 239.8.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mratibu wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) Wilaya ya Kibaha Bw. Harry Godson
alisema kuwa mpango huo wa kuzipatia kaya duni ulikuwa wa majaribio na
utafikia mwisho Julai mwaka huu.

Bw. Godson alisema kwamba, mpango huo umeonesha mafanikio makubwa kwenye
vijiji 12 katika kata sita ambazo ni Tumbi, Soga, Kikongo, Kwala,
Magindu na Gwata kwa kuwa walengwa ni wazee wenye umri zaidi ya miaka 60
na watoto chini ya miaka 18 wanaosoma shule za msingi pia watoto chini
ya miaka mitano.

“Kila kaya inapatiwa shilingi 10,200 kwa wazee na watoto 5,001 kila
mwezi, kwa walengwa walio kwenye mradi huo unaotekelezwa kwenye wilaya
tatu nchini ambazo ni Kibaha, Bagamoyo za Mkoa wa Pwani na Chamwino
mkoani Dodoma,” alisema Bw. Godson.

Alisema kuwa, masharti wanayopewa kwa wazee ni kuhudhuria kliniki japo mara moja kwa mwaka, watoto chini ya miaka 18 wanaosoma shule za msingi wahudhurie darasani angalau kwa asilimia 80 kwa mwaka na watoto
chini ya miaka mitano wapelekwe kliniki mara sita kwa mwaka.

“Katika mpango huu tumepata mafanikio makubwa kwa walengwa ambapo
wazee wameweza kupata matibabu na kutibu magonjwa yaliyokuwa
yakiwasumbua, ufaulu wa wanafunzi umeongezeka na mahudhuria yamekuwa
juu, kipato cha kaya kimeongezeka na uchumi wa vijiji husika nao
umepanda,” alisema Bw. Godson.

Naye Mratibu wa mpango huo Bw. Costa Kauki alisema kuwa mbali ya mafanikio pia wamekumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na umbali wa benki kwa ajili ya kuhifadhia fedha, baadhi ya kaya zisizostahili kuwa kwenye mpango huo kutaka kujumuishwa.

“Kaya zinazonufaika na mpango huu ambao sasa utakuwa wa nchi nzima na
vijiji vilivyosalia, ni zile ambazo zina kipato duni, kula mlo mmoja,
kushindwa kupeleka watoto hospitali, shule na kushindwa kuwahudumia,”
alisema Bw. Kauki.

Bw. Kauki alisema kuwa watu wanaonufaika hutambuliwa kupitia kamati ya
mradi na baadaye hupitishwa na mikutano mikuu ya kijiji husika ambao wao
wanawatambua hata hivyo mradi huo unafadhiliwa na wadau wa maendeleo kwa
kushirikiana na Serikali Kuu.

No comments:

Post a Comment