15 June 2012
Taifa Stars yapaa Msumbiji *Rais Kikwete awapa baraka zake
Na Elizabeth Mayemba
TIMU ya Taifa (Taifa Stars) imeondoka nchini leo kwenda Msumbiji kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya nchi hiyo 'Mambas' kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Mechi hiyo inatarajia kuchezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa ulioko Zampeto nje kidogo ya jiji la Maputo kuanzia saa 9 mchana kwa saa za huko.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameitakia kila la kheri timu hiyo ili ifanye vizuri, huku akiwapongeza kwa ushindi katika mechi yao iliyopita dhidi ya Gambia, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Akikabidhi bendera ya taifa kwa Stars, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik, alisema anaimani timu hiyo itaiwakilisha nchi vyema katika michuano hiyo na Watanzania wapo nyuma yao.
"Mkumbuke kuwa mnakwenda Msumbiji kuiwakilisha nchi, hivyo macho na masikio ya Wanzania wote yapo kwenu kuona mtavuna nini huko, kwa mchezo mzuri mliouonesha mechi iliyopita dhidi ya Gambia bila shaka na huko mtatuwakilisha vizuri," alisema.
Alisema matokeo mazuri waliyoonesha katika mchezo uliopita isiwe ni nguvu ya soda na nidhamu, ambayo wanatakiwa kuionesha huko na ushindi kwao uwe wa kwanza.
Pia Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete, ameitakia kila la kheri timu hiyo na kuitaka iwakilishe vyema nchi.
"Wakati nakuja kuiaga timu ya taifa, Rais ametoa salamu zake kuwa anawatakia kila la kheri ili mfanye vizuri na matokeo ambayo yalipita dhidi ya Gambia yamemfurahisha na anawapongeza sana," alisema.
Naye Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen alisema ili kuitoa 'Mambas' kwenye michuano ya Afrika ni lazima timu yake ishinde mechi hiyo.
Alisema maandalizi katika kikosi chake yalikwenda vizuri ingawa ana wachezaji watatu ambao ni majeruhi, kipa Mwadini Ali na mabeki Nassoro Masoud 'Cholo' na Waziri Salum.
Iwapo Taifa Stars itaitoa Msumbiji katika raundi ya mwisho itapangiwa moja kati ya timu 16 zilizocheza Fainali za AFCON zilizofanyika Januari mwaka huu katika nchi za Gabon na Equatorial Guinea.
Katika mechi ya kwanza dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Dar es Salaam, Februari 29 mwaka huu timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment