15 June 2012
Mbunge aibana serikali muswada wa ushauri
MBUNGE wa Moshi Mjini, mkaoni Kilimanjaro, Bw. Philemon Ndasambulo (CHADEMA), ameitaka Serikali kulieleza Bunge ni lini italeta muswada wa sheria ya Sera ya Taifa ya Ushauri kwenye Viwanda ili iweze kutumika na kuinufaisha nchi kiuchumi.
Bw. Ndesambulo aliuliza swali hilo bungeni mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali na majibu.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Bw. Stephen Wassira, alisema Serikali ilianza kuandaa mchakato wa sera hiyo ili kuwezesha wataalam elekezi kuishauri Serikali mambo ya kiuchumi na kijamii.
Alisema ulijadiliwa na wadau katika hatua mbalimbali na baada ya kukubaliwa, Aprili 2004 ulipelekwa katika Baraza la Mawaziri.
Baraza hilo lilijadili waraka, kukubalina na kumshauri Rais ili aweze kuusaini na kuwa sera rasmi. Ushauri mwingine waliotoa ili kutekeleza sera hiyo, lazima kianzishwe Chama cha Washauri elekezi ili kitumike kama Sekretarieti ya Baraza la Taifa ambapo Ofisi ya Rais, Mipango na Uwezeshaji, ichukue jukumu la kuandaa mpango mkakati wa sera haraka iwezekanavyo na kuhakikisha inatekelezwa kwa faida ya Watanzania.
Alisema kutokana na mabadiliko ya muundo wa Serikali ambao ulitangazwa Februari 2008, baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakisimamiwa na kutekelezwa na Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, yalihamishiwa katika Wizara nyingine.
Aliongeza kuwa, hivi sasa utekelezaji wa sera hiyo unaenda sambamba na Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008, kwa kuhusisha vyombo vya vitatu ambavyo ni Baraza la Ushauri wa Masuala ya Kazi, Uchumi na Jamii.
Mchakato wa kuandaa rasimu ya sheria ya uanzishwaji Baraza la Kitaifa la Huduma na Ushauri, unafanyiwa kazi pamoja na kupata maoni ya wadau mbalimbali chini ya utaratibu wa Wizara ya Kazi na Ajira.
Kwa kuzingatia maoni ya wadau, Serikali itafanya tathmini ya namna kuendelea na utekelezaji wa sera hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment