15 June 2012

Redd's Miss Kigamboni kulamba 500,000



Na Victor mkumbo

MSHINDI wa kwanza wa taji la urembo la Kitongoji cha Kigamboni mwaka huu 'Redd's Miss Kigamboni City 2012', atazawadiwa sh. 500,000 katika mashindano yatakayofanyika leo katika ukumbi wa Navy Beach, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mratibu wa mashindano hayo, kutoka kampuni ya K&L Media Solutions, Somoe Ng'itu alisema maandalizi yote yamekamilika  na warembo wote wako tayari kwa kinyang'amyiro hicho.

Mratibu huyo alisema mshindi wa pili atazawadiwa  sh. 350,000, wa tatu sh. 300,000, wa nne na watano wataondoka na cha sh. 200,000 kila mmoja na wengine saba waliobaki watapatiwa kifuta jasho sh. 150,000 kila mmoja.

Alisema mgeni rasmi katika mashindano hayo atakuwa ni diwani wa kata ya Kigamboni, Dotto Mawa ambaye ametoa mchango mkubwa katika kufanikisha kinyang'anyiro hicho.

Aliongeza kuwa ili kuboresha shindano hilo bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma na msanii na mchekeshaji mahiri hapa nchini, Mpoki watatumbuiza kwenye kinyang'anyiro hicho.

"Tumeboresha zaidi mashindano ya Redd's Miss Kigamboni kwa mwaka huu ambapo warembo wote wana sifa na tunatarajia kuwapata wawakilishi wazuri katika mashindano ya Redd's Miss Temeke pamoja na Redd's Miss Tanzania 2012," alisema.

Aliwataja warembo watakaochuana kuwa ni Susanne Jeremiah, Agness Goodluck, Elizabeth Boniface, Dorothea Kessy, Esther Albert, Edda Silyvester, Sophia Martin, Doreen Kweka, Khadija Kombo, Linnah David, Rosemary Peter na Winnie Karaya.

Aliwashukuru wadhamini ambao wamejitokeza kusaidia mashindano hayo ambao ni Redd's, Dodoma Wine, Hope Country Hotel, Screen Masters, Nobro Collections, Times FM na Kitwe Traders.

Aliongeza kuwa warembo watakaoshika nafasi tatu za juu wataungana na wenzao kutoka vitongoji vya Kurasini na Chang'ombe, ili kuwania taji la Kanda ya Temeke baadaye mwaka huu.

No comments:

Post a Comment