15 June 2012

Good Hope kutoa mafunzo ya ukocha



Na Mhaiki Andrew, Songea

SHIRIKA lisilokuwa la Kiserikali la Good Hope Sports Club la mkoani Ruvuma lina mikakati ya kutoa mafunzo ya ukocha na waamuzi kwa wanafunzi wa shule za Sekondari, ikiwa na lengo la kuibua na kuendeleza michezo mkoani hapa.

Akizungumza mjini hapa juzi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Joseph Mapunda alisema mafunzo hayo yatawalenga wanafunzi wa shule hizo kidato cha kwanza hadi cha tatu ili kuwapatia taaluma ya michezo, badala ya kutegemea makocha kutoka nje ya mkoa kufundisha.

Alisema shirika hilo, limejiwekea malengo endelevu katika kusaidia kuinua michezo ambapo alidai baada ya kukamilika kazi hiyo kwa shule za sekondari pia mafunzo hayo yatatolewa kwa vijana wa shule za msingi kuanzia darasa la tano, ili wajengeke na uelewa kabla ya kuchaguliwa kuanza kidato cha kwanza.

Mapunda alisema kabla ya kuanza kwa utoaji wa mafunzo ya ukocha kwa wanafunzi hao, bodi ya shirika hilo imekutana na kuweka mikakati itakayowezesha kufanikiwa kwa kupendekeza shule za kuanzia, badala ya shule zote kwa pamoja kwa kutumia kanda za kielimu mkoani Ruvuma.

Alisema katika mapendekezo yao, wamekubaliana wataanzia na shule za sekondari katika wilaya mbili za Songea na Namtumbo kabla ya kuamia wilaya nyingine za Nyasa, Mbinga na Tunduru kwa mafunzo hayo ya ukocha na waamuzi ambapo yamelekezwa kutolewa kwa michezo 11 ikiwemo soka, netiboli, ngumi, riadha na mpira wa wavu.

Mkurugenzi huyo alisema programu hiyo ya mafunzo itaanza kutolewa baada ya na kuvutiwa na kituo cha michezo cha Twalipo cha Jijini Dar es Salaam, kilivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa mafunzo ya ukocha na waamuzi kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.

No comments:

Post a Comment