14 June 2012

Migogoro ya ardhi inaweza kupoteza amani tuliyonayo



MIGOGORO ya ardhi imekithiri katika maeneo mbalimbali nchini, kusababisha umwagaji damu, kuhatarisha amani na utulivu tulionao kutokana na umuhimu wake.

Ni wazi kuwa migogoro hiyo imegawanyika katika makundi mawili, moja likihusisha wakulima na wafugaji, jingine linahusisha wananchi na wawekezaji.

Kimsingi migogoro inayohusisha wananchi na wawekezaji inachangia wananchi kuichukia Serikali yao na kuharibu mali.

Katika maeneo mengi yaliyohusishwa na migogoro ya ardhi, tayari kumetokea vurugu zilizosababisha uvunjifu wa amani na kusababisha vifo vinavyoweza kuzuilika.

Vurugu hizo pia zimetokea katika maeneo ambayo wananchi walioheshimiana muda mrefu, wameamua kuvunja udugu wao kwa sababu kasi ya Serikali kumaliza migogoro husika haiendani na tatizo lililopo.

Hatua zinazochukuliwa na Serikali ni zile za kujaribu kutuliza hasira za wahusika jambo linaloweza kutuletea maafa makubwa baadaye.

Sisi tunasema kuwa, migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji inatokana na makundi hayo kutotengewa maeneo.

Mtu akipata eneo mahali popote anajenga, kulima au kufuga kwa sababu Serikali haijachukua hatua stahiki ya kutenga maeneo na matumizi yake.

Ili kuepuka mapigano ya mara kwa mara na kutunza mazingira, umefika wakati wa Serikali kutenga maeneo ya kilimo, ufugaji, makazi ya watu na yale ya wazi.

Maofisa ardhi ni miongoni mwa watu wanaochangia migogoro hiyo kwa kuuza maeneo zaidi ya mara moja hivyo kusababisha jamii kugombana hata kuchukiana.

Sababu kubwa inayochangia maofisa hao kusababisha migogoro hiyo ni tamaa ya fedha mbali ya kujua wazi kuwa wanachokifanya ni kinyume na maadili ya kazi zao.

Ardhi ni mali ya mwananchi na Serikali hivyo kila upande unapaswa kushirikishwa wakati wa kuuza au kumtafuta mwekezaji.

Umefika wakati wa maofisa hao kubadilika na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kupunguza migogoro hii ambayo inaweza kuharibu historia ya nchi yetu.

No comments:

Post a Comment