07 June 2012
Mawakala watatu wamgombea Okwi *Simba wataka euro 500,000 kumwachia
Na Zahoro Mlanzi
NI zali limedondoka, ndivyo utakavyothubutu kusema baada ya Mawakala watatu kutoka nchi mbalimbali kumuhitaji mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Uganda 'The Cranes' na Simba, Emmanuel Okwi akacheze soka la kulipwa Ulaya.
Lakini klabu ya Simba, imeweka wazi kwamba ipo tayari kumwachia nyota huyo kama wakiwa wameweka kitita cha euro 500,000 na si vinginevyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage alisema wamepokea ofa kutoka kwa mawakala watatu ambao wanafanya kazi na wakala Ali Selehe wa Zanzibar kwamba wanamuhitaji mshambuliaji huyo.
"Mawakala hao wanataka Okwi akacheze soka la kulipwa katika nchi za Seribia, England au Australia lakini kati ya hao wakala anayetaka Okwi akacheze Australia ndiye ambaye tunaendelea kufanya naye mazungumzo.
"Tayari ameshatuma maelezo ya awali ambayo yanapitiwa na mwanasheria wake na wanamuhitaji kipindi hiki, lakini hao wengine bado hawajaweka wazi ni lini wanamuhitaji," alisema.
Alisema watakuwa tayari kumruhusu Okwi kwenda popote kwa zaidi ya euro 500,000 kwani wachezaji wao kwa sasa wapo juu kiuchezaji, hivyo dau hilo ni kwa Okwi na ikitokea kwa mwingine watazungumza nao.
Aliongeza kuwa ukiachana na Okwi, pia kuna wachezaji wengine watatu wa timu yake ya vijana (U-20), wakati wowote wanakwenda nchini Ujerumani kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.
Mbali na hilo, pia alijibu maswali kuhusu usajili hususani wa mchezaji Kelvin Yondani ambaye inadaiwa amesaini na Yanga pia, ambapo alisema: "Yondani ni mali yetu na ameshasaini mkataba mwingine, hivyo wanaosema kasaini sehemu nyingine hilo ni la kwao."
Alisema si hilo tu, wanajua vitu vingi vinazungumzwa kuhusu kocha wao, Milovan Cirkovic lakini alithibitisha kwamba wameshamalizana naye na kwamba muda si mrefu atarejea nchini kuendelea kuinoa timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Kagame.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment