19 June 2012

Lisa Jensen kuwakilisha Tanzania Miss World



Na Victor Mkumbo

MNYANGE Lisa Jensen, ndiye atakayewakilisha Tanzania katika mashindano ya urembo ya Miss World 2012, yatakayofanyika Inner Mongolia nchini China mwaka huu.

Lisa aliibuka kidedea katika mashindano madogo ya Redd's Miss Tanzania, yaliyofanyika juzi katika Ukumbi wa 327 Dar es Salaam.


Mrembo huyo aliibuka mshindi baada ya kuwashinda wenzake tisa, ambapo mashindano yalishirikisha warembo 10 ambao waliwahi kushiriki fainali za Miss Tanzania zilizopita.

Katika mashindano hayo ya Redd's Miss Tanzania, yalikuwa tofauti na ilivyozoeleka ambapo warembo hawakuulizwa maswali ila walikuwa wanatoa mada tofauti tofauti kuhusu upeo wao na jinsi ya kuisaidia jamii.

Baada ya kuibuka mshindi Lisa alizawadiwa sh. milioni 2, kugharamiwa gharama zote za safari pamoja na kambi ya mwezi mmoja ambayo itakuwa Dar es Salaam, kabla ya kwenda China katika mashindano ya Miss World 2012 na gharama zote zitalipwa na Kampuni ya Lino Agency ambayo ndiyo inayoandaa Miss Tanzania.

Warembo walioshiriki katika mashindano hayo ni Gloryblaca Mayowa, Hamisa Hassan, Queen Saleh, Christine Willium, Pendo Laizer, Lisa Jensen, Mwajabu Juma, Neema Saleh, Jenifer Kakolaki na Stella Mbuge.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Hamisa Hassan huku Pendo Laiser akishika nafasi ya tatu.

Katika mashindano hayo kulikuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa kikundi cha ngoma za asili cha Wanne Stars pamoja na Saluti Dancers.

No comments:

Post a Comment