01 June 2012
Kibaha kususia kuibua miradi, changamoto ya barabara kilio
Na Mwandishi Wetu, Maili Moja
WAKAZI wa Mtaa wa Ungindoni Kata ya Maili Moja wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani wameiomba Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuifanyia matengenezo Barabara ya Sheli Maili Moja Shule ya Msingi ambayo haijatengenzwa tangu mwaka 2009 hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kuibua miradi mipya.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti mjini Kibaha jana, wakazi hao walisema kuwa barabara hiyo imekuwa ikipitika kwa shida kutokanana mashimo mengi na kipindi cha mvua hali imekuwa mbaya zaidi.
Walisema kuwa, waliibua mradi wa barabara kwenye mkutano wa mtaa ikiwa
kama ni kero na kupeleka halmashauri kwenye bajeti ya mwaka 2010 na
kuandika barua ya kukumbushia bajeti ya miaka miwli iliyofuata, lakini
hadi sasa hakuna kilichofanyika.
“Ilifika wakati tukajichangisha fedha kwa ajili ya kukarabati sehemu korofi, kwani barabara ilikatika kabisa na kukawa hakuna mawasiliano kabisa, lakini wananchi tulijitolea na kuweka kalavati na kurejesha mawasiliano,” Alisema Bw. Mussa Juma miongoni mwa wakazi hao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa huo Bw. Geofidor Nombo alisema kuwa
wananchi waliibua mradi huo wa barabara hiyo na kupeleka sehemu husika
ikiwa ni pamoja na vikao vya kata na halmashauri, lakini toka wakati
huo hawajafanikiwa.
“Tuliandika barua za kukumbushia kwenye bajeti za mwaka 2011 na 2012 ambapo wananchi walisema hawataibua miradi mingine hadi huo utakapotekelezwa kwani ni kero kubwa kwao,” alisema Bw. Nombo.
Naye Mhandisi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Bw. Ezekiel Kunyaranyara
alisema kuwa, kwenye bajeti inayoishia Juni mwaka huu barabara hiyo
haijatengewa fedha zozote.
“Barabara hiyo imetengewa fedha kwenye bajeti ya mwakani, ambapo kiasi
cha shilingi milioni mbili na barabara hiyo ina urefu wa kilomita mbili na
itajengwa kwa matengenezo ya kawaida yaani kiwango cha changarawe,”
alisema Bw. Kunyaranyara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment