27 June 2012

El Merreikh, Red Sea zakwama Kagame Cup


Na Mwandishi Wetu

TIMU za El Merreikh ya Sudan na Red Sea ya Djibouti, zimeshindwa kuthibitisha ushiriki wao mpaka sasa katika michuano ya Kombe la Kagame.

Michuano hiyo imepangwa kuanza kutimua vumbi Dar es Salaam kuanzia Julai 14 mpaka 29, mwaka huu ambapo Yanga ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo.


Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema timu nyingi zimethibitisha lakini za Sudan na Eritrea mpaka sasa hazijatoa taarifa zozote.

"Timu za hapa nyumbani Simba, Yanga na Azam tayari zimethibitisha siku nyingi zilizopita lakini, El Merreikh na Red Sea mpaka sasa zipo kimya kwa hiyo hatujui kama zitashiriki," alisema Osiah.

Pia alizungumzia kuhusu kituo kingine cha michuano hiyo ambacho kinatakiwa kiwe Mwanza, alisema walipokea maombi hayo lakini waliotaka kituo kiwe huko bado kuna vitu hawajakamilisha.

"Tunapenda kituo kiwe huko lakini katika taarifa yao waliyotuletea kuna vitu vimekosekana, hivyo tumewarudishia watuhakikishie baadhi ya vitu hivyo kama vitakwenda sawa ndipo tujue la kufanya," alisema.

Alisema timu nyingi zinapenda kuchezea Dar es Salaam, hivyo kama kituo kikiwa mikoani ni lazima masuala ya msingi kama usafiri wa kwenda na kurudi uwepo na si wa kusuasua.

Droo ya michuano hiyo inatarajiwa kupangwa kesho pamoja na ratiba zingine zikiwepo za timu zilizoalikwa kwa mwaka huu, pamoja na jinsi zitakavyowasili.

Mpaka sasa timu za Platinum ya Afrika Kusini, Vital Club ya DRC Congo na nyingine ya Zimbabwe zimeomba zishiriki katika michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment