14 June 2012
Chanzo cha ajali za ndege chatajwa
Na Willbroad Mathias
TATIZO la ubovu wa miundombinu katika viwanja vya ndege na ukosefu wa mafunzo kwa marubani, linadaiwa kuwa chanzo kikuu cha ajali nyingi za ndege zinazotokea nchini.
Wadau wa sekta ya usafiri wa anga nchini, waliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wao uliolenga kujadili na kutafuta njia mbadala ya kuimarisha usalama wa safari za ndege.
Wakichangia mada inayohusu changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, wadau hao walisema ajali nyingi za ndege nchini, zinasababishwa na ufinyu wa miundombinu katika viwanja.
Walisema pamoja na kuboreshwa kwa njia za ndege zinazotumika wakati wa kuruka au kutua, viwanja vingi nchini vimezungukwa na mazingira yasiyo salama.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini, kutoka Wizara ya Uchukuzi, Bw. John Nyamwihura, alisema ipo haja ya kuboreshwa miundombinu hiyo ili kuleta ufanisi.
Akizungumzia tatizo la uhaba wa mafunzo ya marumbani nchini Bw. Nyamwihura alisema sekta hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto hizo baada ya Serikali kujitoa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Alisema awali Serikali ilikuwa ikibeba jukumu la kugharamia masomo ya marubani tofauti na sasa.
“Hali hii inachangia kuwa na marubani wengi vijana tena wa kigeni tofauti na Tanzania ambayo marubani wengi wazee, enzi ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere, tulikuwa na utaratibu wa kusomesha marubani katika nchi mbalimbali,” alisema Bw. Nyamwihura.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Chama cha Wasafirishaji wa Anga (TAOA), Bw. Eva Jackson, alisema ipo haja ya kuwepo uwazi katika kuchunguza vyanzo vya ajali za ndege nchini.
“Hivi sasa ukienda katika taarifa za Mamlaka ya Anga (TCAA), hakuna taarifa za matukio ya ajali au ya usalama licha ya kuripotiwa zaidi ya mara 10,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Fadhili Manongi, alisema ajali za ndege nchini zimepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Alisema mwaka huu kumetokea ajali moja tofauti na miaka iliyopita ambayo zilikuwa zikitokea mara kwa mara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
NI AIBU KUSEMA MARUBANI WANA UPUNGUFU WA UTAALAMU JE MUNAFANYIA MAJARIBIO MAISHA YA WATANZANIA SI AFADHALI MUNGENONG'ONA MUNATANGAZIA DUNIA KUWA MARUBANI WENU NI VIHIYO HIVI MTALII GANI ATAPANDA NDEGE INAYOENDESHWA NA MTANZANIA NI HIVI HIVI ALIYEKUWA MWANASHERIA WA KENYA CHARLES M. NJONJO MIAKAYA[1963-1979] ALIKUWA HAPANDI NDEGE ILIYOENDESHWA NA MTU MWEUSI TANZANIA SASA TUNAKUBALIANA NAYE
ReplyDelete