12 June 2012

Akili za wasomi zitumike kuendeleza sekta ya elimu


Na Willbroad Mathias


ILI Tanzania iwe na maendeleo endelevu lazima kujenga utamaduni wa kujiendeleza kimasomo hasa katika fani za biashara na ujasiriamali.

Kwa kufanya hivyo, watakuwa wamejirahisishia mazingira ya kumudu ushindani unaolikabili soko la ajira ndani na nje ya nchi. Hakuna njia ya mkato zaidi ya watu kuwekeza katika sekta ya elimu.

Changamoto hiyo ndiyo imewafanya watanzania wengi kuwekeza katika elimu.

Mkuu wa Chuo Cha Biashara cha Aseki cha mkoani Dodoma,  Bw. Omari Kiputiputi, wakati akizungumzia maendeleo ya elimu na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo pamoja na umuhimu wa ujasiriamali.

Bw. Kiputiputi anasema ni mhitimu wa Shahada ya Elimu ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1979 na pia ana Shahada ya pili ya usimamizi wa biashara akiwa amebobea zaidi upande wa masoko MBA aliyopata mwaka 1998.

Anasema baada ya kuhitimu shahada ya ualimu wa masomo ya sayansi mwaka 1979 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliajiriwa na Chuo cha Biashara Dar es Salaam CBE na kufanya kazi katika chuo hicho kwa miaka 31 ambapo alistaafu kwa mujibu wa sheria mwaka 2010.

Anasema, miaka 10 ya mwisho licha ya kuendelea na kazi ya ufundishaji alipewa dhamana ya kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha CBE Dodoma.

Bw.Kiputiputi anasema, akiwa katika nafasi hiyo alikikuta kikiwa na wanafunzi 183, lakini hadi anaondoka aliacha wanafunzi zaidi ya 4,000.

"Uwezo wa kampasi ile ni wanafunzi 200 tu, lakini tuliweza kufanya yote haya kutokana na stadi za kijasiriamali," anasema.

"Nilipokea kampasi ile ikiwa inaendesha programu moja tu ya stashada katika fani tatu tu yaani uhasibu, uendeshaji biashara na uboharia, lakini nimeiacha kampasi ikiwa inaendesha programe tatu, cheti, stashahada na shahada katika fani tano za uhasibu, uendeshaji biashara, masoko, uboharia na TETAMA yaani Teknolojia ya Taarifa na Mawasiliano," anasema.

Anasema kwa kuwa alifanya kazi kwa bidii, utiifu, ubunifu na uadilifu mkubwa, alipostaafu mwajiri wake alimpa zawadi nyingi, ikiwemo cheti cha utumishi uliotukuka hivyo anawahimiza watanzania kujituma zaidi katika kufanya kazi.

Bw.Kiputiputi anasema, hata hivyo akiwa bado yupo kazini wazo lake kubwa lilikuwa ni kuanzisha chuo chake binafsi ili aweze kuwasaidia watanzania kufaidi matunda ya elimu yake.

Anasema kuwa hata hivyo ndoto zake zilikamilika mwaka jana baada ya kufanikiwa  kuanzisha chuo chake binafsi  cha Biashara cha Aseki cha mkoani Dodoma, ambapo anaahidi kutoa wahitimu bora wanaoweza kujiajiri wenyewe au hata kuajiriwa kila pembe ya dunia.

Anasema  kozi zinazofundishwa kuwa ni pamoja na cheti cha uhasibu, cheti cha uendeshaji wa biashara na cheti cha manunuzi na ugavi.

Bw. Kiputiputi anasema kwa upande wa stashahada wanatoa katika uendeshaji wa biashara, stashahada katika uhasibu na stashahada ya manunuzi na ugavi.

Anaongeza kuwa mwanafunzi yeyote aliyemaliza kozi ya cheti NTA 4 inayoendana na fani hizo kutoka kwenye chuo chochote kilichosajiliwa na NACTE au aliyemaliza kidato cha sita na kupata angalau 'pass' moja au 'subsidiary' pass mbili anaweza kujiunga na kozi ya stashahada.


“Tunajitahidi chuo hiki kiwe cha kipekee hapa nchini kwa kutoa wahitimu bora katika menejimenti, ujasiriamali na ujuzi kupitia mafunzo, utafiti, utumishi wa umma na huduma za kijamii katika kanda hii na hata nje ya mipaka ifikapo mwaka 2020,” anasema.

Anasema chuo kitahakikisha kinawaandaa wanafunzi katika misingi bora ya uendeshaji bora wa biashara wenye mafanikio makubwa kwa kuwatumia wanataaluma waliobobea katika gani husika.

Bw. Kiputiputi anasema chuo kimepata usajili kamili kutoka NACTE na hiyo inamaanisha kwamba mtu yeyote atakayesoma kwenye chuo hicho na kufanikiwa kupata cheti kitatambuliwa rasmi nchini na duniani kote.

Anasema ili kufikia malengo hayo wamedhamiria kutoa elimu ya kiwango cha juu na kwa gharama ambazo watanzania wengi wataweza kuzimudu katika kozi za usimamizi wa biashara, uhasibu na fedha, masoko, ugavi na manunuzi, masomo ya  kompyuta na kozi zingine zinazoendana na masomo hayo.

Anafafanua kuwa, iwapo wahitimu watapata mafunzo ya kiwango cha hali ya juu itarahisisha kupata maendeleo endelevu, kwani nchi itakuwa na wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbali kama zinazotolewa na chuo hicho.

Ili Aseki ifikie malengo hayo, anasema wamepanga kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu moja, kwa kuzingatia weledi wa taaluma, uadilifu, ubunifu, huduma kwa wateja na uwajibikaji wa pamoja.

Bw. Kiputiputi anawaomba watanzania kuchangamkia fursa ya kuanzishwa kwa chuo hicho kwa kuwa elimu ni ufunguo wa maisha pia hazina pekee kwa urithi wa baadaye.

Anasema wazazi au walezi ambao wana vijana waliomaliza kidato cha nne na kukosa sifa ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano wasikate tamaa ili mradi tu wawe wamefaulu na kupata angalau alama tatu za D, hivyo wanaweza kujiunga na chuo hicho.

“Akija hapa sisi licha ya kumpa stadi muhimu za maisha tutampa pia sifa za kuweza kujiunga na chuo kikuu chochote nchini ndani ya miaka mitatu, tutampa stadi za kuweza kujiajiri yeye mwenyewe au kuajiriwa baada miaka hiyo mitatu ya kwanza endapo atashindwa au ataamua kutoendelea na masomo zaidi,” anasema, Bw. Kiputiputi.

Anasisitiza kuwa, “Tumepania kuwa kituo kilichotukuka, yaani kituo bora kwa kutoa elimu, mafunzo na stadi katika nyanja za biashara, uendeshaji na ujasiliamali kupitia mafunzo, utafiti, huduma kwa umma na shughuli za nje ya chuo katika kanda hadi kufikia mwaka 2020.”

Bw. Kiputiputi anasema walimu wote wa chuo hicho wana angalau shahada ya kwanza na stashahada ya juu, hivyo wahitimu wa chuo hicho wanakuwa na viwango vya elimu inayokubalika katika fani mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Dkt. Richard Mushi, anawahimiza watanzania kuwa na utamaduni wa kuanzisha miradi kwa ubia kwani ndiyo njia pekee ya kuanzisha miradi mkubwa.

Anasema wengi hawapendi kuanzisha miradi ya ubia kwa kutoaminiana, lakini aliwatoa hofu kuwa walioanzisha chuo cha ASEKI kwa ubia wamefanikiwa na chuo kinazidi kusonga mbele siku hadi siku.

“Waanzilishi wa chuo hiki wanastahili pongezi. Baraza linaona fahari kuongoza chuo hiki kwani licha ya kuanzishwa na watu binafsi, chuo kimetimiza masharti yote ya msingi ya kuandikishwa yaliyowekwa na Baraza la Vyuo vya Elimu ya Ufundi NACTE na ndiyo maana kimepata usajili kamili,” anasema Dkt. Mushi.

Anasema baraza la chuo limedhamiria kuona wakufunzi wa chuo hicho wanapata elimu ya ngazi ya juu zaidi ili waweze kumudu majukumu yao ipasavyo na wawe na viwango vinavyokubalika popote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani, Bw. Balozi Job Lusinde anasema Baraza lake limepania kuhakikisha linasimamia viwango vya juu vya taalum ili wahitimu watakaotoka Aseki wawe watu wa kupigiwa mfano.



No comments:

Post a Comment