11 May 2012
Zimbabwe kamili kuivaa Twiga Stars
Na Mwali Ibrahim
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Zimbabwe Rosemary Mugdza amesema kikosi chake kipo kamili kukabiliana na timu ya Taifa ya wanawake 'Twiga Star' katika mchezo wake wa kirafiki wa kimataifa utakaochezwa kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha huyo alisema, walikuwa wakisaka timu ya kucheza nayo ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi yao na mechi ya Nigeria ambapo waliamua kuichagua Tanzania kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao.
"Twiga ni timu nzuri na yenye uwezo na ndio maana tuliona ni timu ya kuchuana nayo tukiwa katika maandalizi ya mchezo wetu huo kwani tunaimani tutapata mazoezi ya kutosha," alisema.
Aliongeza kuwa kwa upande wa maandalizi wamejiandaa vya kutosha hivyo wanaimani kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri katika mchezo wao ujao.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa Shirikisho la soka nchini (TFF) Bonifance Wambura akizungumza kwa niaba ya kocha wa Twiga, Boniface Mkwasa alisema hata kwa upande wao mchezo huo utakuwa ni mchezo mmoja wa kimataifa ambao ni kwa ajili ya mechi ya maandalizi ya kuivaa Ethiopia Mei 26, mjini Adis Ababa.
"Huu ni mchezo wa kwanza wa kimataifa wa kirafiki kwa ajili ya kujiweka sawa kwani timu hii itacheza mchezo mwingine wa kirafiki Mei 20 ambapo kwa sasa tunatafuta timu ya kucheza nayo," alisema.
Alisema, timu hiyo ilikuwa mkoani Mwanza ikimalizia ziara yake ya kucheza michezo mbalimbali ya kujipima nguvu ambapo sambamba na mkoa huo pia walicheza mchezo mmoja mkoani Dodoma.
Wambura alisema, kwa upande wao wako tayari kukabiliana na timu hiyo kwani wanaijua vizuri walishawahi kuchuana nayo katika mashindano ya All African Games mwaka jana.
Alitaja viingilio katika mchezo huo kuwa VIP A ni sh. 10,000, VIP B sh. 5,000 na viti vingine vikiwa ni sh. 1,000 ambapo wanaimani mashabiki watajitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo.
.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment